Tuesday, 24 June 2014

Vinara wa tindikali, mabomu mbaroni


NA MWANDISHI WETU
MTANDAO hatari wa uhalifu unaohusishwa na kuwamwagia watu tindikali na ulipuaji mabomu, umetiwa mbaroni mjini Zanzibar.
Habari za kuaminika zimesema watuhumiwa saba ambao wanatajwa kuwa vinara wa matukio hayo, walitiwa mbaroni juzi baada ya kufuatiliwa nyendo zao kwa muda mrefu.
Kabla ya kukamatwa, inadaiwa mtandao huo ulipanga kufanya tukio lingine la kihalifu visiwani humo na kwamba polisi walifanikiwa kunasa  mawasiliano hatari ya washirika wa mtandao huo.
Chanzo chetu hicho, kilisema mtandao huo, unadaiwa kuhusika na maujia ya aliyekuwa Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Machi, mwaka jana.
Pia kilisema mtandao huo unahusishwa na tukio la umwagaji wa tindikali kwa baadhi ya wananchi, wakiwemo watalii wawili raia wa Uingereza, Katie Gee na Kristie Trup.
Agosti, mwaka jana, watalii hao ambao walikuwa walimu wa kujitolea katika Kituo Maalumu cha Sober House, walimwagiwa tindikali Mji Mkongwe, Zanzibar.
Pia mtandao huo unahusishwa na tukio la kummwagia tindikali Sheha wa Shehia ya Tomondo, Mohamed Omari Said. Tukio hilo lilitokea Mei, mwaka jana.
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, mtandao huo wa uhalifu unahusishwa na ulipuaji wa bomu uliotokea hivi karibuni Zanzibar na kusababisha kifo cha mhubiri wa amani, Sheikh Ahmed Haidari Jabir.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omari Makame, alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa saba wanaodaiwa kuhusika na matukio ya uhalifu yaliyotokea hivi karibuni visiwani humo.
Makame alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi mjini Zanzibar na kwamba walisafirishwa hadi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam, kwa ajili ya kuhojiwa zaidi.
“Ni kweli tuliwakamata watu saba wanaodaiwa kuhusika na matukio ya uhalifu visiwani hapa na tayari tumewasafirisha kwenda Dar es Salaam ambako ndio kwenye kikosi kazi na wanahojiwa huko,” alisema.
Alisema tukio la ulipukaji wa bomu uliotokea Zanzibar linasimamiwa na Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam na kwamba mtuhumiwa yeyote atakayekamatwa atakabidhiwa kwa kikosi hicho.
Hata hivyo, alisema hali ya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar ni mzuri na amewataka wananchi kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji mali kama kawaida.
Makame alisema polisi wamejipanga vya kutosha kukabiliana na tukio lolote litakalojitokeza visiwani humo.
Katika salamu zake za pole kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, Rais Jakaya Kikwete alisema tukio hilo linapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na wapenda amani wote nchini na kwamba ni kitendo hicho si cha ustaarabu na hakikubaliki katika dunia ya sasa.
Rais Kikwete aliwataka watu kuwa wastarabu, wavumulivu na kuheshimu imani na mitazamo ya watu wengine hata kama hawakubaliani nayo.
Aliliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki waliohusika katika tukio hilo lisilo la kistaarabu.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Kamishna Isaya Mngulu, aliwasili Zanzibar na kutembelea eneo la tukio ambapo alitoa maelekezo ya kusaidia kukamatwa kwa watuhumiwa wa tukio hilo.
Katika tukio hilo la bomu, watu saba walijeruhiwa na kulazwa hospitali ya Al-rahma, Zanzibar.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru