NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
UONGOZI wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), umeishitaki bodi yake ya zamani kwa kumega viwanja viwili na kuvimilikisha kwa wamiliki wengine kinyemela.
Umesema viwanja hivyo kwa sasa vimejengwa majengo makubwa ikiwemo hoteli ya kisasa na kanisa.
Mkurugenzi wa Miliki na Miradi wa AICC, Paul Ndosa, alitoa shutuma hizo mbele ya bodi mpya huku akisema kuwa madudu hayo yalifanywa miaka iliyopita na kwamba hakuna taarifa zozote.
Alisema maeneo yaliyomegwa kinyemela na bodi hiyo ya kituo hicho ya wakati huo imeonekana kubariki utoaji wa ardhi hiyo kwa wamiliki hao ingawa haikuwa sahihi.
Maeneo hayo kwa sasa yamejengwa hoteli ya Themi Suites na eneo lingine Kanisa la Glory Land.
Taarifa hizo zilimshangaza mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo Dk. Khamis Kigwangwala, ambaye alitaka maelezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Elishilia Kaaya, iwapo ni kweli maeneo hayo yamemegwa ambapo mkurugenzi huyo alikiri.
ìEti mkurugenzi ni kweli maeneo hayo yamemegwa na umefuatilia ni kwa nini hayo yalifanyika maana hayaelezeki kabisa,î alihoji Dk. Kigwangala.
Kutokana na swali hilo, Kaaya alijibu kuwa ni kweli yamemegwa na watu hao kugawana ingawa uamuzi huo ulifanywa na bodi iliyomaliza muda wake kipindi kirefu kilichopita ambapo hakukua na ufuatiliaji wowote uliofanyika.
ìNi kweli jamani waheshimiwa maeneo hayo yamemegwa ingawa bodi hiyo iliridhia kinyemela, lakini msije mkaninyonga yalimegwa zamani kipindi hata mimi nikiwa shule ya msingi sikuwepo,î alijibu Kaaya.
Pia, aliwaeleza wajumbe wa bodi hiyo mikakati mbalimbali ya kukamata soko la utalii wa mikutano hapa nchini ambapo alisema kituo kina mpango wa kujenga vituo vya mikutano katika kanda zote za nchi.
Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Balozi Abdul Mshangama, alisema ujenzi wa vituo hivyo ni muhimu kutokana na soko kubwa lililopo hapa nchini kwa sasa.
Alisema kwa sasa Tanzania bado haina kituo kikubwa chenye uwezo wa namna hiyo zaidi ya kile cha Dar es Salaam, ambacho bado hauna uwezo wa kutosha kupokea kiasi kikubwa cha wageni na hata vifaa.
Aidha aliutaka uongozi wa kituo hicho kutafuta wadau wa maendeleo watakaoweza kuwekeza na kuendesha shule na hospitali kwa kushirikiana na kituo hicho badala ya kuacha maeneo mengi yanayomilikiwa na kituo hicho yakiwa wazi.
Monday, 16 June 2014
Uongozi wa AICC ‘waingizwa mjini’
03:05
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru