Tuesday, 10 June 2014

Mapya ya UKAWA yafichuka



  • Mabilioni yamwagwa kwa kususia bunge

NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
UMOJA wa Vyama vyenye wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano (TCD), utaitisha Baraza la Chama hicho kujadili hatua ya wabunge wa vyama vya CHADEMA, NCCR- Mageuzi na CUF kususia Bunge la Katiba.
Wiki iliyopita, vyama hivyo vilisusia mkutano ulioitishwa na umoja huo ili kuwahoji viongozi wa vyama hivyo kueleza sababu za wabunge kususia vikao.
Pia ulitaka maelezo ya tuhuma za baadhi ya wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kudaiwa kuwa hulipwa sh. 450,000 kwa siku wanaposusia vikao vya Bunge la Katiba.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Philip Mangula, aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, Kamati ya Ufundi ya TCD iliitisha mkutano huo ili kujadili na kusikiliza sababu ya vyama hivyo kususia Bunge la Katiba.
Alisema TCD ilipendekeza iandaliwe faragha ambayo viongozi wa vyama wangejipa muda wa kutafakari hali na mwenendo huo.
‘’Nia yetu ilikuwa ni kujua nini hasa kiliwakwaza wenzetu hadi wakatoka nje na kupata muafaka wa matatizo hayo ili tusonge mbele na Katiba ambayo ni muhimu kwa taifa,” alisema Mangula.
Aliongeza kuwa faragha hiyo ingehusisha watu mashuhuri ili wajumuike na wajumbe wa TCD kupata ufumbuzi wa suala hilo, lakini suala hilo halikufanikiwa baada ya UKAWA kutotokea kwenye kikao hicho.
“Wajumbe wengine wa TCD pia walitaka kusikia kauli ya UKAWA kuhusu tuhuma zilizotolewa kuwa wanafadhiliwa na baadhi ya vyama na taasisi kubwa barani Ulaya ili wasusie mchakato huo.
‘’Na habari hizo zimedai kuwa wameshapokea kiasi cha sh. bilioni 1.7 na baadaye wana ahadi ya kupatiwa zingine kutoka kwa wafadhili, haya ni mambo tuliyotaka kuyafahamu,” alisema.
Mangula, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, alisema pia kuna habari kuwa wajumbe hao wa UKAWA wasipoingia bungeni katika mchakato huo wa katiba, hulipwa sh. 450,000 kwa siku.
Alisema kwa kuwa wahusika wakuu wa tuhuma hizo hawakuwepo kwenye kikao hicho cha TCD ili kutoa ufafanuzi, wajumbe wameadhimia kuitisha kikao cha Baraza  la Taifa la Vyama vya Siasa linalojumuisha vyama vyote 22 vyenye usajili wa kudumu ili kuendelea kutafakari hatma ya mchakato katika awamu ya pili ya bunge.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa kikao cha TCD hakutaja tarehe rasmi ya baraza hilo kukutana ila alisema ni mapema kabla ya kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru