NA DOROTHY CHAGULA, MUSOMA
MKAZI wa Musoma mkoani Mara,
Emmanuel Lucas, anashikiliwa na polisi
kwa tuhuma za kumbaka kwa nyakati tofauti binti yake wa miaka 19 (jina
linahifadhiwa) na kumwambukiza ukimwi.
Lucas (52), anatuhumiwa kufanya
kitendo hicho kuanzia mwaka 2007 na
kumsababishia binti yake kupata maambukizi ya ukimwi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mara, Paul Kasabago, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akimbaka binti yake huyo
mara kwa mara hadi kupata ujauzito, ambapo mtoto aliyezaliwa alifariki dunia.
Alisema binti huyo baada ya
kujifungua, alipimwa afya yake na kugundulika kuwa ni mwathirika wa virusi vya
ukimwi, hivyo kutoa taarifa polisi mjini
hapa.
Wakati huo huo, mtoto Catherine
Emmanuel (4) wa kijiji cha Masinono wilayani Butiama, amepotea katika mazingira
ya kutatanisha tangu Juni 22, mwaka huu, akiwa mikononi mwa baba yake wa
kufikia, Emmanuel Dinda.
Alisema kabla ya kupotea, mtoto huyo alisindikizwa
nyumbani kwao na mtoto mwenzake Nelea Emmanuel (9), ambaye alimkabidhi kwa baba
yake huyo na wakati anaondoka kurudi kwao alisikia mwenzake akiwa analia.
Kwa mujibu wa Kamanda Kasabago,
Nelea alimweleza bibi yake kuwa alimwacha mwenzake analia huku mlango ukiwa
umefungwa, lakini bibi yake aliichukulia kuwa hali ya kawaida kwa mtoto
kuadhibiwa.
Alisema baadaye mama mzazi wa
Catherine, Anastazia Emmanuel, wakati akirejea kutoka kisimani alikutana na
mumewe akiwa amebeba kiroba chenye kitu kizito ndani yake akienda kusikojulikana.
Alisema mama huyo, alipofika
nyumbani alikuta mwanawe hayupo, huku kukiwa na kinyesi na ndala ndani ya
nyumba, ndipo alipoanza kumtafuta.
Polisi inamshikilia Dinda ili
aeleze mazingira ya kupotea kwa Catherine.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru