Monday, 16 June 2014

Meneja Tanzanite One atoroka nchini


Na Mwandishi Wetu, Arusha 
MENEJA Mauzo wa Kampuni ya Tanzanite One, Jacques Beytel (39) maarufu ‘Kibakuli’ raia wa Afrika Kusini aliyekamatwa wiki iliyopita kwa kosa la kufanya kazi nchini bila ya kibali, ametoroka.
Habari za kuaminika zimesema kuwa Kibakuli alitoroka kwa kusaidiwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti tukio la kukamatwa kwa Kibakuli na maofisa wa Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha, kwa kosa la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Daniel Namomba, alikiri kukamatwa kwa meneja huyo na kueleza kuwa leo atatoa taarifa kamili.
Hata hivyo, habari zimeeleza kuwa Beytel alitoroka nchini Ijumaa usiku na kusindikizwa na mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzanite One (jina tunalo) hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kimanjaro (KIA).
Hata hivyo, kuna utata mkubwa wa kuondoka kwa kwa kigogo huyo wa Tanzanite One kiholela kwani, imeelezwa kuwa hakukabidhi ofisi na muda mfupi kabla ya kukamatwa alikabidhiwa madini ya Tanzanite yenye thamani ya dola za Marekani milioni moja (sh. bilioni sita).
Habari za kuaminika zinasema kuwa kutoroka kwa Beytel kumetokana na baadhi ya wakubwa wa Tanzanite One kuficha maovu na kwamba, hofu imetanda kuhusu mahal yalipo madini hayo.
Namomba alipopigiwa simu kuhusiana na taarifa za kutoroka kwa Beytel, kwanza alisema yuko mkoani Tanga kwenye msiba na kuwa hana taarifa juu ya hilo na kuwa ni uongo mkubwa.
Pia, alimtaka mwandishi kwenda ofisini kwake Jumanne (kesho) kwa ajili ya kupata taarifa za Beytel.
“Niko safarini Tanga kwenye msiba sina taarifa za kutoroshwa kwa Baytel, unachonieleza ni uongo mkubwa na mtuhumiwa yupo nitatoa taarifa Jumanne mara nitakaporejea kutoka Tanga subiri,’’ alisema.
Hata hivyo, wakati Mkuu wa Uhamiaji akisema taarifa za kutoroka kwa meneja huyo ni za uongo, Ofisa Uhusiano ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanzanite One, Doto Medard, alikiri kuondoka kwa Beytel.
Alisema utaratibu mzima wa kumrudisha kwao Afrika Kusini umefanywa na serikali na uongozi wa Tanzanite One, haukuhusika kwa chochote.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mederd alisema meneja huyo ameondoka bila kukabidhi ofisi kwa uongozi wa Tanzanite One.
Alipoulizwa kuhusu suala la kutoweka na madini hayo, alishindwa kuthibitisha wala kukanusha kama aliondoka na madini yenye thamani ya sh. bilioni 16).
‘’Ni kweli Beytel ameondoka nchini juzi, sisi kama Tanzanite One hatuhusiki kabisa na kuondoka kwake, taratibu zote za kumrudisha kwao zimesimamiwa na serikali,” alisema
Kuhusu kumdhamini polisi, Mederd alisema binafsi hakumdhamini ila alipewa taarifa juu ya kukamatwa kwake kama kiongozi mkuu wa kampuni hiyo kwa sasa.
Kwa mara ya kwanza, Beytel alifika nchini mwaka 2002 na kufanya kazi Tanzanite One kwa nafasi hiyo na alifukuzwa mwaka 2008 kwa tuhuma za kudaiwa kuiba madini ya mabilioni ya shilingi, lakini ghafla alirudi tena kufanya kazi hadi alipotiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya kazi bila kibali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru