Na Ahmed Makongo, Bunda
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani
Mara, kimesema baadhi ya watumishi wa serikali mkoani humo, wanaihujumu
serikali pamoja na ilani ya uchaguzi ya Chama.
Katika madai yake hayo, CCM
imesema watumishi hao wanafanya hivyo kwa kutokuwajibika ipasavyo katika
kutekeleza majukumu yao ikiwa pamoja na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher
Sanya, alitoa shutuma hizo kwa nyakati na maeneo tofauti, wakati akihutubia
vikao vya ndani na kwenye mikutano ya hadhara kwenye tarafa za Kenkombyo,
Nansimo na Chamriho.
Sanya alisema baadhi ya watumishi
wa serikali wanaihujumu serikali na ilani ya Chama, kwa kushindwa kusimamia
utekelezaji wa ilani hiyo ipasavyo. Alsiema hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya
miradi ya maendeleo kuwa chini ya kiwango na kutokukamilika kwa wakati, hivyo
wananchi kuichukia serikali yao.
“Hapa tunagundua kwamba ni kweli baadhi ya watumishi wa serikali ndio wanaoihujumu serikali na Chama chetu na wanafanya makusudi kabisa kutuharibia. Kama Chama tunasema hatutaki mambo hayo yaendelee kuwepo, wanatupatia wakati mugumu sana kukinadi Chama kwa wananchi,” alisema.
Alisema baadhi ya watumishi hao wanaihujumu pia serikali
ya CCM kwa kutokutoa huduma
zinazostahili kwa jamii hasa katika
sekta za afya, maji, elimu na miundombinu.
Akitoa mfano katika sekta ya afya,
alisema baadhi ya waganga na wauguzi wamekuwa wakiuzia wajawazito na watoto
kadi za kliniki ambazo hutolewa bure na serikali, hali ambayo inaichafua
serikali ya CCm.
Alisema katika sekta ya ujenzi
baadhi ya watumishi wa serikali wamekuwa wakishirikiana na wakandarasi kuhujumu
miradi inayotekelezwa na hivyo kujinufaisha na fedha za miradi hiyo, kinyue cha
sharia.
Aliongeza kuwa hali hiyo imekuwa
ikikichafua chama hicho, kwani ndicho chenye serikali na kwamba CCM mkoani
Mara, haitavumilia hali hiyo iendelee kuwepo kwa sababu fedha zinazotolewa
kwenye miradi hiyo zinatokana na kodi ya wananchi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru