Tuesday, 10 June 2014

Kinondoni inaongoza kwa ufuska-Madiwani


NA RACHEL KYALA
KIKAO cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni jana kilitikiswa vikali baada ya kuzuka kwa malalamiko ya kuwepo kwa vitendo vya ufuska vilivyoshamiri katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam.
Idadi kubwa ya madiwani hao wameelezea kushuhudia na kusikitishwa na vitendo hivyo, hususan vya ngono na kuiomba serikali kutofumbia macho suala hilo walilosema linafaa kuitwa janga la kitaifa.
Madiwani hao waliyataja maeneo mbalimbali katika manispaa yao, ambayo yamekuwa yakiendesha vitendo hivyo kuwa ni Msasani, Sinza, Kinondoni na Oysterbay na kuliita jambo hilo kama sababu ya kuporomoka kwa maadili katika jamii, kichocheo cha ngono ikiwemo maambukizi ya ukimwi.
Diwani wa kata ya Msasani, Kulthum Segamiko, alisema aliwahi kupatiwa fedha kiasi cha sh. 20,000 na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaaa wa Msasani ili kwenda kushuhudia mambo yanayoendelea katika moja ya klabu ya usiku.
“Nilikwenda na mambo niliyoyaona kwa kweli yanasikitisha, kwani kila Jumatano wanawake ndio hujiuza kwa kunengua viuno na kuingiza chupa sehemu za siri na siku za Alhamisi ni siku za wanaume mashoga kujinadi kwa kufanya mambo machafu,” alisema.
Aliitaja klabu nyingine, ambayo ipo Kinondoni na kusema kuwa mahali hapo huendeshwa mchezo ujulikanao kama ‘kangamoko’, ambapo mwanamke huvaa kanga moja nyepesi na kumwagiwa maji na kuita tendo hilo ndembendebe, akisha loana ndipo huanza kucheza michezo ya aibu.
Renatus Pamba, Diwani wa Kata ya Sinza, ameiomba serikali kupiga marufuku vitendo viovu vinavyofanywa na machangudoa katika eneo lake, hususan Sinza Mori, barabara ya Meeda kwani wanawake hucheza uchi huku wakijinadi kwa wanaume nyakati za jioni na usiku.
“Eneo hili ni kuanzia kituo cha mafuta cha Bigborn pale Mori. Hii ni picha mbaya sana kwa taifa kutokana na vitendo vya aibu vinavyofanywa na machangudoa hao,” alisema. 
Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Uchumi, Afya na Elimu wa baraza hilo, Othman Chipeta, alisema ataandamana na viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kutembelea maeneo hayo, ingawa aliwataka madiwani kutoa maagizo kusimishwa haraka kwa kabu hizo katika maeneo yao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru