Monday, 30 June 2014

TPB yawapiga jeki Kyela


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepokea hundi ya sh. milioni 5 kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Kyela walioathirika na mafuriko ya mvua za masika.
Mvua hizo zilitokea mwanzoni mwa mwaka huu na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi na miundombinu.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika Makao Makuu ya TPB, ambapo Dk. Mwakyembe, ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, alishukuru kwa mchango huo na kueleza kuwa utatumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema mvua ziliharibu miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na madarasa na vyoo, hivyo kuwafanya watoto kushindwa kupata elimu kwa kadri inavyotakiwa.
Mwakyembe alisema tathmini ya awali hadi kukamilika kwa ujenzi huo inaonyesha jumla ya sh. bilioni mbili zinatakiwa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi, alisema msaada huo umelenga kusaidia ukarabati wa majengo ya shule zilizoathirika kwa kiasi kikubwa, ili watoto waweze kurejea darasani.
ìTunatambua uharibifu uliotokana na mvua hizo ni mkubwa na changamoto zinazoikabili wilaya hiyo bado ni nyingi, ili kurudisha hali ya maisha ya wakaazi hao kama zamani,  tunaahidi kuwa nanyi bega kwa bega kuwasaidia,” alisema.
Alisema Benki ya Posta ni taasisi ya fedha ya umma ambayo siku zote ipo katika mstari wa mbele kuisaidia serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazotokea ndani ya jamii.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru