Tuesday, 24 June 2014

CUF yashindwa kuweka ukomo wa uongozi


NA WAANDISHI WETU
LICHA ya kufanya marekebisho ya Katiba, Chama cha CUF kimeshindwa kugusa vipengele juu ya ukomo wa uongozi ndani ya chama hicho. 
Badala yake wamefanya mabadiliko ya kuwaongezea madaraka zaidi Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, ambao sasa wana uwezo wa kuteua mjumbe wa kamati ya utendaji ya taifa.
Awali, wajumbe wa Kamati ya Utendaji walikuwa wanatokana na mkutano mkuu wa taifa, ambao ulikuwa unawachagua kwa kuwapigia kura na si kuwateua.
Akitangaza baadhi mabadiliko hayo, Naibu Mkurugenzi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema kupitia mkutano mkuu wa chama hicho ulioanza juzi, Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad, amewasilisha mapendekezo ya kuboresha chama hicho kwa kuongeza ngazi utawala, kutoka wilaya pekee, hadi majimbo na mikoa.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi, Salim Biman, alisema pia mkutano huo unajadili kupunguza idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu kutoka 700 hadi takribani wajumbe  300.
Hata hivyo, viongozi wa chama hicho hawakuweka wazi  kama kuna wajumbe waliopeleka mapendekezo ya kuboresha katiba zaidi ya Hamad, na kama vipengele vya uongozi vimeguswa kwa namna yoyote au la.
“Niko nje ya mkutano, nikikwambia naweza kukupotosha, subiri tujadili halafu tutakachotoka nacho, tutawajulisha waandishi wote wa habari,” alisema Biman.
Kiongozi mwingine (jina linahifadhiwa), akijibu kwa kubabaika alisema hajakiona kipengele chochote cha mabadiliko ya katiba kinachohusu uongozi na hakumbuki kama kipo kwenye nyaraka walizopewa. 
Mkutano huo unaoendelea leo, utaingia katika kipengele cha ajenda ya uchaguzi, kwa ajili ya kuchagua viongozi wa ngazi za kitaifa huku Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahimu Lipumba na Hamad wakionekana kung’ara kwa ajili ya kushika hatamu kwa miaka mingine mitano ijayo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru