NA HAMIS SHIMYE
CHADEMA inaendelea kuingia katika mpasuko, baada ya mamia ya wanachama wa chama hicho kuandamana na kupeleka barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Wanachama hao wakipeleka barua zao katika ofisi hizo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kaliua, Joram Mmbogo na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke, Joseph Yona.
Wanachama hao walikuwa wamebeba mabango mbalimbali yaliokuwa yakisomeka ‘Mbowe, ruzuku umeshindwa kuisimamia, ukipewa nchi si utauza migodi na mbuga za wanyama?’
Akizungumza baada ya kumkabidhi barua hiyo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema wamepokea na wataifanyia kazi.
“Tumeipokea na tutaifanyia kazi. Ndani ya muda mfupi tutatoa jibu kama walivyotuombana, hatuwezi kuidharau.”
Aliongeza kuwa: “Kawaida ndani ya wiki mbili tunatakiwa tutoe jibu lakini ikiwa ni jambo kubwa na linahitaji kupewa ufafanuzi wa haraka, hatutasita kutoa taarifa,’’ alisema.
Kwa upande wake, Mmbogo alisema wamepeleka barua kwa Msajili kueleza uvunjifu wa katiba unavyofanyika ndani ya chama hicho.
Alisema: “Tunamwomba Msajili aifanyie kazi barua yetu pamoja na kuitaka CHADEMA iitishe mkutano wa Baraza Kuu.”
Mbali na kupeleka barua hiyo kwa msajili, wanachama hao wakiongozwa na Mmbogo walipeleka barua nyingine katika Ofisi ya CAG kuelezea ufisadi wa fedha za ruzuku ndani ya chama hicho.
Alisema Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, wanahusika moja kwa moja na ubadhirifu wa fedha za ruzuku ya chama.
“Tunamwomba CAG atoe taarifa ya ukaguzi kwa wanachama ili tujue chama kinafanya nini na je, kina haki ya kuzungumzia ufisadi maeneo mengine?,’’ alisema na kuongeza: “Dk. Slaa ajibu hoja na asilete maneno ya vioja na kuwaita watu ni wahuni kwa kuwa wanachama wana hoja za msingi katika masuala yao muhimu.
Hata hivyo, safari ya wanachama hao kwenda kwa CAG nusura iingie doa baada ya polisi kuvamia msafara wao na kuwaonya kuwa hawataki mkusanyiko wa watu wengi.
Kitendo hicho kilimfanya mmoja wa viongozi wa msafara huo, Yona kutii sheria na kumweleza Ofisa wa Polisi kuwa watatawanyika eneo zilipo Ofisi za CAG.
Wanachama hao waliondoka eneo hilo na baadaye Yona, alirudi peke yake na kuikabidhi barua.
“Tunafanya hivi ili kuondoa ubadhirifu ndani ya chama chetu. Niko tayari kufungwa endapo CAG atatoa taarifa ya kusema hakuna ubadhirifu ndani ya CHADEMA,’’ alisema.
Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, alipoulizwa alisema wataitisha mkutano na wanahabari kuzungumzia suala hilo.
Wednesday, 25 June 2014
Mtikisiko CHADEMA
08:50
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru