Sunday 22 June 2014

Ajali ya magari manne yaua sita Dar

NA MWANDISHI WETU

WATU sita wamefariki dunia mjini Dar es Salaam na wengine 12 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari manne.

Ajali hiyo ambayo ilitokea saa 7:30 mchana, ilihusisha daladala mbili, lori na gari dogo aina ya Land Rover Discover ambapo ilitokea katika eneo la Lugalo njiapanda.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema, ajali hiyo ilisababishwa na daladala lililokuwa likitoka Ubungo kwenda Tegeta lenye namba za usajili T 441 CKT ambalo lilihama njia na kupanda tuta kisha kuliparamia daladala lingine lenye namba T 377 BEF.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, baada ya gari hilo kuliparamia daladala hilo, nalo liliserereka na kuligoga lori ambalo halikuwa na namba, ambapo lori hilo nalo liliigonha Land Rover Discover yenye namba za usajili T 454 AWZ.
Mashuhuda hao walisema, watu waliofariki ambao juhudi za utambuzi zilikuwa zinaendelea hadi jioni ni abiria wa daladala hizo, ambapo watatu ni wanawake na wanaume watatu na kwamba, majeruhi wengi wako katika hali mbaya. 
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zilisema, ajali hiyo ilisababishwa na dereva wa daladala hilo kukosa maarifa ya kiudereva, suala lililosababisha gari hilo kuhamia upande wa pili wa barabara.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa kinondo, Camilius Wambura, alisema majeruhi wote wako katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo wanaendelea kupatiwa matibabu.
Alisema, jeshi hilo linamsaka dereva wa daladala lililosababisha ajali hiyo ambaye alitoweka baada ya kuisababisha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru