Friday 27 June 2014

Serikali yacharukia viwanda vya nyavu


WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amesema viwanda vyote vinavyotengeneza nyavu haramu zinazotumika katika shughuli za uvuvi vitachukuliwa hatua za kisheria.


Dk. Kamani amesema hatua hizo pia zitachukuliwa kwa wafanyabiashara wanaouza nyavu hizo na wale wanaozinunua na kuzitumia katika uvuvi kwa vile kufanya hivyo ni kosa kisheria.



Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini-CCM), aliyetaka kujua kwa nini serikali inashindwa kuwachukulia hatua wamiliki wa viwanda vinavyotengeneza nyavu hizo na wanaoziuza kwa vile wanafahamika.



"Wanaotengeneza, wanaoziuza, wanaozinunua na kuzitumia katika uvuvi, wote wanafanya makosa kisheria na watashughulikiwa," alisema.



Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri wa Maendeleo  ya Mifugo na Uvuvi, Kaika Ole Telele, alisema serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha wavuvi wadogo kwa kuhakikisha kuwa zana na vyombo vya uvuvi vinapatikana kwa bei nafuu.



Alisema katika jitihada hizo, serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu za uvuvi na vifungashio.



Telele alisema pia kuwa injini za uvuvi, malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake, hupewa punguzo la kodi ama kufutiwa kodi kabisa ili kuwawezesha wavuvi kumudu bei za vifaa hivyo.



Naibu Waziri alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014, Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), kupitia Dirisha la Kilimo, imewezesha miradi minne ya uvuvi yenye thamani ya sh. bilioni 1.5 katika halmashauri za Sumbawanga, Ukerewe, Ilemela na Muleba.



Alisema miradi hiyo imewezesha upatikanaji wa boti nne za uvuvi na vifaa vya kuhifadhia samaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, boti sita za uvuvi Ukerewe, boti 28 za uvuvi, injini za boti 20 na boti moja ya doria Ilemela.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru