Friday 27 June 2014

Akana kumfanyia unyama yaya wake



SUBIRA SAID NA EVA MBESELE, TSJ
MWANAMKE Amina Maige, mkazi wa Dar es Salaam, anayedaiwa kumfanyia ukatili msichana wake wa kazi, kwa kumng'ata meno sehemu mbalimbali na kumsababishia majeraha amekana mahakamani kutenda kitendo hicho.
Amina alikana kumfanyia hivyo, Yusta Kashinde, jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, mbele ya Hakimu Yohana Yongolo, wakati akisomewa maelezo ya awali.
Akimsomea maelezo hayo, Wakili wa Serikali, Tumaini Mfikwa, alidai Amina (42), mkazi wa Mwananyamala, wilayani Kinondoni, anafahamiana na Yusta ambaye alikuwa mfanyakazi wake wa ndani.
Tumaini alidai Yusta alianza kufanya kazi za ndani kwa Amina kuanzia Januari, 2012 hadi Juni 3,  2014.
Alidai mshitakiwa huyo katika kipindi chote, alikuwa akimng'ata Yusta kwa meno na kumsababishia majeraha.
Wakili huyo, alidai mshitakiwa alikamatwa  Machi 4, mwaka huu na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kupandishwa kizimbani Juni 12, mwaka huu.
Baada ya kumsomea maelezo hayo mshitakiwa huyo ambaye yupo rumande tangu alipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza kutokana na upande wa Jamhuri kupinga dhamana, alikubali jina lake, umri, mahali anapoishi na kwamba anamfahamu Yusta.
Mshitakiwa aliomba mahakama impatie dhamana kwa kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Hata hivyo, Hakimu Yongolo alikataa ombi hilo na kumtaka mshitakiwa kuwasiliana na uongozi wa Magereza ili aweze kupatiwa matibabu.
Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Julai 10, mwaka huu, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.
Umati wa watu ulifurika mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia shauri hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru