Monday 30 June 2014

CCM Kibaha yaweka hadharani msimamo


NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kibaha Mjini, kimesema wanachama wake watakaoongoza kura za maoni pasipo mizengwe, watateuliwa kuwania uongozi katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
Kimesema kitakabiliana na wagombea wote wasiokubali kushindwa, ambao mara nyingi wamekuwa chanzo cha kuendeleza makundi na kuleta matatizo kwenye uchaguzi.
Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Abdallah Mdimu, alisema hayo juzi kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani alipokuwa akifunga mafunzo ya viongozi hao yaliyofanyika mjini hapa.
ìSuala la wagombea wanaokubalika halina mjadala kwa kuwa CCM imejipanga kuhakikisha wanachama wanaokubalika kwa wananchi wapewe nafasi ili kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima.
ìTunahitaji kushinda uchaguzi, hatufanyi majaribio, tunataka kuendelea kushika dola, dola inaanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo ni lazima tusikilize wananchi  wanahitaji nini,î alisema.
Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Pwani, Dk. Zainab Gama, aliwataka viongozi wa CCM kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na wananchi.
Dk. Zainab aliwataka wana CCM kuacha tabia kuwalalamikia viongozi wanaofanya kazi zao vizuri kwani watakatishwa tamaa na mwisho wa siku CCM ndio itakayopata hasara.
Aliwashangaa wanaopiga kelele pale diwani au mbunge anapotekeleza majukumu yake ya kazi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru