Monday 16 June 2014

Vita dhidi ya ujangili yashika kasi


NA WILLIAM SHECHAMBO
JITIHADA za serikali katika mapambano dhidi ya vitendo vya ujangili nchini, zimechukua sura mpya baada ya kukabidhiwa helkopta na Taasisi ya Howard Buffet Foundation ya Marekani, kwa ajili ya shughuli hiyo.
Helikopta hiyo ni moja kati ya ahadi alizowahi kuzitoa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwa serikali, kama jitihada zinazofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na wadau katika kuhifadhi wanyamapori na maliasili.
Makabidhiano ya helikopta hiyo yalifanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) na kushuhudiwa na Waziri Nyalandu, Balozi wa Marekani nchini Mark Childress, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa na Mwenyekiti wa Kudumu wa Kamati ya Bunge ya Aridhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nyalandu aliishukuru Howard Buffet Foundation na kwamba Helikopta hiyo imekuja wakati muafaka, ambapo kwa mujibu wa takwimu mwaka uliopita tembo 20,000 waliuawa barani Afrika, huku asilimia 80 ya mauaji hayo yakifanyika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema pamoja na jitihada kadhaa zilizofanywa na serikali, utaratibu mpya wakutumia anga kufanya doria mbugani wanaotaka kuuanzisha, anaamini utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la ujangili uliokithiri nchini.
Kwa mujibu wa Nyalandu, helikopta hiyo aina ya Robinson R 44 II, ni moja kati ya nyingie mbili ikiwemo aina ya Bell ambayo ni kubwa zinazotarajiwa kuingizwa nchini kwa shughuli za uhifadhi kwenye mbuga na hifadhi za taifa.
Kwa upande wa Balozi Childress, alisema Marekani itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Tanzania kwenye jitihada za uhifadhi wa wanyamapori na maliasili, kwa kutafuta njia sahihi zitakazoweza kusaidia kukomesha vitendo vya ujangili hususan wa tembo kwenye hifadhi mbalimbali nchini.
Alisema wanyamapori na maliasili ni mali za serikali zenye manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi, hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazooneshwa na serikali yao ikiwemo kutoa taarifa mara wanapotilia shaka baadhi ya watu wanaoweza kujihushisha na ujangili kwa namna moja au nyingine.
Msigwa, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada zinazoonyeshwa na Nyalandu katika kukabiliana na ujangili, kuboresha utalii na kutimiza ahadi na kauli anazozitoa bungeni.
Alisema hakuna anayebisha kuwa ujangili ni tatizo kwa maendeleo ya taifa na kwamba, ilitakiwa kupatikane utatuzi wa haraka kama uliofanywa na wizara kwa kushirikiana na wadau hivyo, tofauti za kiitikadi zinawekwa pembeni na kushirikiana kwa pamoja kufurahia mafanikio hayo yaliyopatikana ili Tanzania iweze kutoka mahali ilipo na ipige hatua zaidi kimaendeleo.
Kwa upande wake Lembeli, alisema wizara inastahili kupongezwa kwa hatua hiyo iliyofikia lakini bila msaada wa wananchi na wadau, hawataweza kufikia malengo iliyojiwekea hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhusika kwa namna yoyote kwenye mapambano dhidi ya ujangili na vitendo vingine vinavyotishia usalama wa wanyamapori na maliasili.
Kwa kuanzia,  helikopta hiyo ambayo ni moja kati za ahadi zilizotolewa na serikali kwenye mapambano dhidi ya ujangili, ambazo kwa ujumla zitakuwa na gharama ya dola za Marekani milioni 5, itakuwa ikifanya doria kwenye mbuga ya Selous.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru