Monday 16 June 2014

UDA kuuza tiketi kwa njia ya mtandao


Na Mwandishi Wetu,
KAMPUNI ya Simon Group Limited inayomiliki Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) imetangaza kuanza mpango wa kuuza tiketi kwa njia ya mtandao ili kuondoa msongmano na adha kwa watumiaji.
Mbali ya hatua hiyo, imesisitiza dhamira yake ya kuboresha sekta ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam licha ya kampeni zinazoendelea kutoka kwa washindani binafsi ikiwa na lengo la kuvuruga mpango unaoendelea wa uwezekezaji katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ili waweze kuitawala biashara ya usafiri.
Kwa mujibu wa taarifa ya UDA, mpango unaendelea wa kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji lenye urahisi katika usafiri kwa kufanya kazi kwa karibu na serikali na jiji.
ìTumeona taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kutoka katika kundi linalojiita ‘Consortium of Concerned Tanzanians International’ wakijaribu kuwafanya watu waamini kila uwekezaji unaofanywa katika kuboresha mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam kupitia UDA, hauna maana.
ìHiii ni hatua inayosikitisha sana, tunajaribu kuuboresha mfumo wa usafiri Dar es Salaam kutoka katika msongamano ili kuwa katika hali inayoridhisha kwa kuongeza idadi ya magari na kuboresha huduma za usafirishaji, lakini watu wengine wanatumia muda mwingi kufanya kampeni zenye lengo la kuhakikisha malengo hayo hayatimii,íí ilisema taarifa hiyo kutoka kwa mwenyekiti ambaye pia  ni Ofisa Mtendaji Mkuu, Robert Kisena.
Aliitaja kampeni hiyo iliyopewa jina la ìKampeni ya Kurudisha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) Mikononi mwa Wananchiî inajaribu kuligeuza mtaji suala la kujivunia umiliki wa kampuni hiyo kwa umma bila ya kuangalia ni vipi kampuni inaweza kusimamiwa kwa namna bora na kufanikiwa kutimiza malengo ya kurahisisha usafiri Dar es Salaam.
Alisema kwamba kampuni yake iliamua kuwekeza UDA baada ya kutangazwa kubinafsishwa kwa sababu Simon Group Limited, ilitaka kuleta mabadiliko yenye maana katika mfumo wa usafiri katika jiji la Dar es Salaam hasa katika mabasi ya abiria na usafirishaji kwa ujumla.
ìMpango wa kuboresha usafiri umeelezwa vizuri katika mipango yetu ya muda mfupi na muda mrefu inayoonyesha ni jinsi gani tuna mpango wa kusimamia mabadiliko haya hatua kwa hatua. Katika mpango wetu pia tumebainisha ni vipi tunajipanga kuihusisha serikali na jiji katika mpango mzima wa usafiri Dar es Salaam. Naamini hii ndio maana hasa ya uzalendo, kufanya kazi na serikali yako ili kutoa huduma bora kwa wananchi wake,íí alieleza Kisena katika taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, Kisena alibainisha kwamba mpango walioudhamiria wa kampuni hiyo kuboresha huduma ya usafiri Dar es Salaam uko pale pale ukihusisha mradi wa kuwa na mabasi zaidi ya 3,000 na mengine ya kifahari 50 yenye viyoyozi na huduma ya intaneti.
Alisema sambamba na mpango huo, kampuni itasimamia sera ya kuwaajiri wataalamu wa hapa nchini badala ya kuwapa wataalamu wa kigeni kazi ambazo Watanzania wanazimudu.
ìKampuni ya Simon Group Limited inamilikiwa na Watanzania, katika hilo nitakuwa mtu wa mwisho kumkubali mtaalamu wa kigeni kuajiriwa  katika nafasi ambayo inaweza kushikwa na Watanzania wenzangu. Kama hatutopata mtaalamu Mtanzania, tutaleta wataalamu wa kuwapa mafunzo Watanzania ili baadaye wazichukue nafasi hizo,” alisema Kisena.
Alisema kwamba tathmini inaonyesha kuwa ili kuwezesha mabasi yapatayo 3000 kufanya kazi hapo baadaye wataalamu wapatao 7800 watahitaji kupewa mafunzo na kuajiriwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru