Thursday 12 June 2014

Moto wateketeza soko Mchikichini


NA WILLIAM SHECHAMBO
TAKRIBAN wafanyabiashara 10,000 wa soko la mitumba la Mchikichini lililoko Ilala, Dar es Salaam, wamepata hasara baada ya mali zao kuteketea kwa moto uliounguza soko hilo usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, moto huo ulizuka majira ya saa 4.00 usiku, kwenye vibanda vilivyoko eneo la katikati ya soko hilo.
Walisema muda mfupi baadae, moto huo ulishika kwenye vibanda vingine na kuanza kusambaa kwa kasi kutokana na uwepo wa bidhaa za nguo zinazopatikana kwa wingi sokoni hapo.
Jumanne Kangogo, ambaye ni mwenyekiti wa soko hilo, alisema taarifa ya tukio hilo aliipata muda mfupi baada ya kuzuka, ambapo alitoka nyumbani na kufika eneo la tukio huku akifanya jitihada za kutoa taarifa kwa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.
Alisema kikosi hicho kiliwasili eneo la tukio saa 5 usiku, na kuanza shughuli ya kuzima moto iliyochukua takribani saa saba, mpaka kufikia alfajiri kutokana na ukali na ukubwa wake.
Kiongozi huyo wa soko alisema hadi sasa hawajajua chanzo cha moto huo wala thamani ya mali zilizoteketea.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, wafanyabiashara wengi wameathirika kutokana na ukweli kwamba hawakuwa na bima ya aina yoyote, hivyo wamepoteza dira ya maisha yao.
“Wafanyabiashara wengi hawana tabia ya kukata bima, huo ndio ukweli. Tunaiomba serikali ituangalie kwa namna moja au nyingine kutokana na janga hili lililotupata,” alisema Jumanne.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa tangu kuanza kwa moto huo, askari wake waliimarisha ulinzi ili kusimamia mali na usalama wa wahanga wa tukio hilo.
Pia alisema wameunda kikosi maalumu kwa kushirikiana na Idara ya Zimamoto na Uokoaji, kuchunguza chanzo cha moto huo, ambao umesababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara hao.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alitoa pole kwa wahanga wa tukio hilo na kusema serikali iko pamoja nao.
Alisema serikali imeona na imetambua kuwa hasara iliyopatikana ni kubwa,
na wameanza kulishughulikia suala hilo, ikiwemo kukutana na Ofisa Masoko wa Manispaa, Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii ili waweze kupata ufumbuzi.
Sambamba na hilo, alisema Mkuu wa Wilaya Ilala, Raymond Mushi, atafanya vikao na kamati yake ya ulinzi na usalama ili wachunguze na kujua chanzo cha moto huo.
Meya huyo alisema pia kuwa eneo hilo litabaki kuwa sehemu ya biashara na si vinginevyo, hivyo wafanyabiashara wawe wavumilivu kusubiri matokeo ya upelelezi unaofanywa juu ya tukio hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru