Tuesday 10 June 2014

Wabunge waibana serikali

  • Wataka bajeti mpya iwe ya utekelezaji si ahadi
  • Misamaha ya kodi kwa vigogo yazidi kupingwa
  • January: Misamaha iwe asilimia moja ya bajeti

NA SELINA WILSON, DODOMA
WABUNGE wameendelea kuikalia kooni serikali juu ya misamaha ya kodi kwa wawekezaji wakitaka ipunguzwe na wengine wakitaka ibuni vyanzo vipya vya ukusanyaji mapato badala ya kutegemea wahisani.
Bajeti Kuu ya Serikali inatarajiwa kusomwa bungeni kesho, ambapo kwa wiki nzima, wabunge wamekuwa wakiibana serikali kuitaka kueleza namna itakavyopata fedha huku suala la misamaha ya kodi na ulegevu katika ukusanyaji mapato likiwa gumzo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wabunge wa majimbo mbalimbali walisema, wanatarajia serikali itakuja na bajeti yenye manufaa kwa Watanzania na sio kuwanufaisha wachache.
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, alisema umefika wakati lazima serikali itambue kwamba hadhi ya nchi imebadilika na hivyo misamaha ya kodi ibadilike.
Alisema mwanzoni wawekezaji walikuwa wakisamehewa baadhi ya kodi kutokana na kutumia gharama kubwa kwenye utafiti wa rasilimali, lakini sasa ni wakati wa ugunduzi hivyo hakuna sababu ya misamaha tena.
“Zamani ilikuwa ni utafiti, hakuna uhakika kama utapata madini, au gesi, lakini sasa tayari mali nyingi zimegundulika, hivyo hakuna sababu ya kuendelea na misamaha mikubwa ya kodi kwa wawekezaji,” alisema.
Alisema anatarajia katika bajeti itakayowasilishwa kesho, itaangalia maeneo muhimu na kuweka utaratibu mpya, ikiwemo mgawo wa fedha za maendeleo kwa wakati.
Ridhiwan Kikwete (Chalinze-CCM), alisema anatarajia serikali itatoa majibu juu ya kilio cha misamaha ya kodi na kueleza mazingira mapya ya ukusanyaji kodi.
Alisema jambo lingine kubwa ni kwamba serikali inapaswa kueleza ni kwa namna gani wataondokana na tatizo la kushindwa kupeleka fedha katika maeneo zinakohitajika na kusababisha miradi ya maendeleo kukwama.
Ridhiwani alisema pia kuna haja ya kuangalia maeneo mapya ya kukusanya kodi kwa kurasimisha wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kama ‘wamachinga’ na ‘mama ntilie’ kwa kuweka utaratibu mzuri wa biashara zao na kukusanya kodi.
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema kuna haja ya kubadilisha mfumo wa upelekaji fedha za maendeleo kwenye maeneo husika na kuhakikisha kunakuwa na uharakishaji ili miradi isikwame.
Kwa upande wa misamaha ya kodi, alisema inabidi ipunguzwe hadi kufikia asilimia moja ya bajeti ili kupanua wigo wa makusanyo ya ndani.

“Natarajia bajeti ya mwaka huu itaweka umuhimu katika miradi ya maendeleo katika maji, umeme na barabara na jambo la muhimu ni kuongeza makusanyo na kupunguza misamaha,” alisema.
Alisema pia lipo tatizo la matumizi ya fedha ambapo miradi inachelewa kutekelezwa wakati fedha zipo na hali hiyo inasababisha gharama za mradi kuongezeka.
Kwa upande wake, Said Mtanda (Mchinga-CCM), alisema hatarajii jambo lolote jipya kwenye bajeti ijayo kwa kuwa utaratibu ni ule ule, serikali inapanga bajeti kubwa wakati haina uwezo wa kuitekeleza.
Alisema ni afhadhali itengwe bajeti ya sh. trilioni 10 na ikatumia kiasi hicho kutekeleza mipango badala ya kupanga kutumia trilioni 14 ambazo hazipo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru