Monday 16 June 2014

UPORWAJI WA SILAHA KITUONI...


Polisi bado njia panda

NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi nchini limesema silaha zilizoporwa na majambazi katika tukio uvamizi wa kituo cha polisi cha Kimanzichana bado hazijapatikana na hakuna mtu anayeshikiliwa.
Tukio hilo lilitokea Juni 11, mwaka huu ambapo majambazi walivamia kituo hicho usiku wa manane na kuua askari mwenye namba D.9887 Koplo Joseph Ngonyani.
Silaha zilizoporwa katika kituo hicho ni Shot gun tatu na SMG mbili za Jeshi la Polisi.
Akizungumza na Uhuru jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema bado wapo eneo la tukio wakiendelea na uchunguzi.
Kamishna Chagonja alisema hadi sasa bado silaha hizo hazijapatikana na hakuna mtu yeyoyote anashikiliwa kufuatia tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chagonja siku ya tukio, zaidi ya watu sita walivamia Kituo Kidogo cha Polisi cha Mkamba na kumshambulia askari huyo na wengine watatu na kutoweka na silaha hizo.
Alisema watu hao walifika kituoni hapo  na kupora shot gun tatu za kirai na SMG mbili za Jeshi la Polisi zikiwa na magazini zenye risasi 30 kila moja.
Silaha hizo zilikuwa kwenye ghala la muda kusubiri kupelekwa kwenye kituo kikubwa ambako ndiko kwenye ghala kuu la silaha.
Aidha, alisema watuhumiwa hao pia waliwajeruhi askari mgambo wawili waliokuwa kituoni hapo ambao ni Venance Francis na Mariamu Mkamba.
Chagonja alisema jeshi hilo litahakikisha watuhumiwa hao pamoja na silaha hizo zinapatikana haraka kabla hazijasababisha madhara kwa raia wengine.
Alitaka wananchi kutoa taarifa kupitia namba ya simu ya mkononi ya 0754 785557 au namba za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei ambayo ni 0715 009953 ili watuhumiwa hao waweze kukamatwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru