Tuesday 10 June 2014

Kanisa lamkana Mzee wa Kanisa


  • Ni anayedaiwa kufuga chatu nyumbani
  • ajipanga kumwadhibu kwa kulichafua 

Na waandishi wetu, arusha
SAKATA la nyoka aina ya Chatu kukutwa nyumbani kwa Mzee wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Monica jijini hapa, Joseph Magesa, limechukua sura mpya baada ya kanisa kumkana kumtambua.
Juzi, waumini na wananchi walikusanyika kanisani hapo kumshughudia Magesa baada ya kuahidi kuwa angefika kula kiapo, lakini hakuweza kutimiza ahadi hiyo na kuzidisha utata.
Hata hivyo, jana kanisa hilo limesema kuwa kamwe halimtambua Magesa kama ni Mzee wa Kanisa na kwamba, hana wadhifa wowote.
Pia, limesema kuwa kanisa hilo halina utaratibu wa kuwa na cheo cha Mzee wa Kanisa kama Magesa alivyodai.
Akizungumza na Uhuru jana, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Simon Tengesi, alisema halimtambua Magesa na kuwa, kitendo chake cha kujitangaza kuwa ni Mzee wa Kanisa hilo ni upotoshaji mkubwa.
Tengesi aliongeza kuwa hata taarifa kuwa Magesa angefika kanisani kula kiapo ili kuudhihirishia umma kutokana na tukio hilo kuhusishwa na imani za kishirikina, alisema pia ni upotoshaji.
Alisema kanisa lake halina utaratibu wa kumuapisha muumini wake kwa kuwa halina mamlaka haya.
ìKuzungumza kula kiapo ni kupotosha huo ni uwongo na kutafuta kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabali, hatuna utaratibu huo kwani ni kinyume na maagizo ya Yesu Kristo," alisema Tengesi.
Pia, alisema kutokana na kanisa kuhisishwa na tukio hilo la Magesa, kwa sasa wanafanya vikao ili kuchunguza lengo halisi la kuguswa pamoja na tukio zima kwa ujumla.
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa huenda mzee huyo akatengwa na kanisa kutokana na kulichafua.
Hata hivyo, Tengesi alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, alisema yeye sio msemaji katika hilo na kuwa hatua hiyo bado haijafikiwa na lolote litakaloamuliwa waumini watajulishwa.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Kaskazini (KDU), Paschal Mrina, alisema wamewahoji watuhumiwa wawili kwa kuhusika na mauaji ya Chatu huyo.
Waliohojiwa ni Philibert Magesa (22) na mfanyakazi wa ndani aitwaye Amos, ambao wote waliohojiwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamanda Mrina alisema kuwa bado wanaendelea kumsaka Magesa na kwamba, muda wowote watakaokanyaga Arusha atakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kuishi na mnyama huyo kinyume cha sheria.
Wiki iliyopita wakazi wa Arusha na viunga vyake kuanzia asubuhi walikuwa wakifurika nyumbani kwa mzee huyo wa kanisa na mfadhili wa kanisa katoliki jimbo kuu Arusha parokia ya Mtakatifu Monica kumshuhudia chatu huyo aliyekadiriwa kuwa na urefu wa mita nne aliyedaiwa kufugwa ndani ya nyumba ya mzee huyo.
Chatu huyo alikuwa amefungwa vitambaa vya aina mbili shingoni vya rangi nyeusi na nyeupe vikiwa na maandishi yasiyofahamika alidaiwa kuzua tafrani ndani ya nyumba hiyo kabla ya kuvunja kioo cha dirisha na kutoka nje.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru