Tuesday 24 June 2014

CHADEMA majanga


NA HAMIS SHIMYE
BAADA ya kujaribu kuficha migogoro nyuma ya kichaka cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), hatimaye bundi wa migogoro ameibuka tena ndani ya CHADEMA.
Kwa muda mrefu sasa, kumekuwemo mvutano kutokana na kile kinachodaiwa ukiukwaji wa Katiba na matumizi mabaya ya madaraka na fedha za chama.
Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya viongozi wakiwemo wa ngazi za juu kuvuliwa uanachama na wengine kutimuliwa. 
Baadhi waliovuliwa uongozi ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Hata hivyo, juzi wanachama wakiwemo wajumbe wa mkutano mkuu wa CHADEMA, walitoa tamko zito wakiutuhumu uongozi wa juu kwa ubadhirifu wa fedha za ruzuku na matumizi mabaya ya madaraka.
Pia leo wanatarajia kuandamana kwenda katika Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa nchini, kuwasilisha malalamiko hayo yakiwemo madai ya ufisadi na ukiukwaji wa Katiba ya CHADEMA.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya CHADEMA, zilieleza kuwa malalamiko hayo yatafikishwa katika ofisi za msajili leo.
Awali, malalamiko hayo yalikuwa yapekelekwe jana lakini ilishindikana kutokana na Msajili (Jaji Francis Mutungi) kutokuwepo ofisini.
“Jana malalamiko yalitakiwa kupelekwa lakini imeahirishwa hadi leo. Lakini tunaiomba ofisi ya msajili iitake CHADEMA iitishe mkutano wa wanachama,’’ alisema mmoja wa wanachama hao.
Uamuzi wa wanachama hao, kupeleka malalamiko katika ofisi ya msajili ni kutokana na chama hicho kushindwa kutisha mkutano wa baraza kuu la chama hicho kama kanuni zinavyotaka.
Katibu wa CHADEMA mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Athumani Balozi, alisema chama kimeshindwa kuitisha mkutano wa baraza kuu kinyume cha katiba.
Alisema Katiba inaagiza kila baada ya miezi 12, Baraza Kuu liitishwe, ambapo lilipaswa kuitishwa kabla ya Februari, mwaka huu, lakini uongozi umekaa kimya.
“Chama kimeshindwa na hata wanachama wanapohoji wanashindwa kupewa majibu ya kina juu ya lini mkutano utaitishwa,’’ alisema.
Alisema CHADEMA inapokea zaidi ya sh. bilioni 10 za ruzuku kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini bado imeshindwa kujiendesha na hata kukosa kitega uchumi.
Balozi alisema wanahitaji mkutano wa baraza kuu, ili kuwataka viongozi wao wakuu, Freeman Mbowe (Mwenyekiti) na Katibu Mkuu, Dk. Willbrad Slaa, kujipima na kujiuzulu nyadhifa zao.
UHURU jana ilifika katika ofisi za msajili, ambapo mmoja wa watumishi wa ofisi hiyo walisema hayupo.
“Mimi si msemaji na msajili hayupo, njoo kesho (leo) anaweza kuwepo atakupa kila kitu maana yeye ndio anajua wageni wake,’’ alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CHADEMA, John Mnyika, alipoulizwa kuhusu madai ya wajumbe hao, alijibu yuko bungeni na kuelekeza atafutwe Ofisa Habari wa Chama hicho, Tumaini Makene.
Hata hivyo, Makene alipoulizwa aliomba apewe dakika tano ili aweze kutoa majibu, lakini alishindwa kufanya hivyo na kila alipopigiwa simu yake iliita bila majibu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru