Friday 27 June 2014

Mabomu yaua 12, yajeruhi watu 137




WATU 12 wameuawa na wengine 137 kujeruhiwa katika matukio tisa ya ulipuaji mabomu yaliyotokea katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Lindi, Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.

Aidha, watu 25 wamekamatwa katika tukio la ulipuaji bomu lililofanyika hivi karibuni katika eneo la darajani kisiwani Zanzibar, ambapo mtu mmoja alifariki. Watano kati ya watu hao, wameshafikishwa mahakamani.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perreira Ame Silima, alipokuwa akijibu swali la Waride Bakari Jabu (Kiembesamaki-CCM), aliyetaka kujua kauli ya serikali kuhusu matukio ya uhalifu wa kutumia tindikali na ulipuaji mabomu yaliyotokea hivi karibuni.

Silima alisema katika juhudi za kukabiliana na matumizi haramu ya tindikali, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkemia Mkuu wa Serikali ya  Muungano na  ya Zanzibar, liliendesha operesheni kubwa ili kupunguza matumizi holela ya tindikali. Alisema operesheni hiyo imeonyesha mafanikio makubwa.

Naibu Waziri alisema kwa sasa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio yaliyotokea katika mikoa hiyo sita, ambapo wataalamu wamefanikiwa kubaini aina za mabomu yanayotumika na nchi yanakoundwa kama silaha za kivita.


"Kwa sasa timu hiyo inaendelea na uchunguzi wa kisayansi ili kubaini waingizaji na walipuaji wa mabomu hayo," alisema.


Silima alisema serikali imejidhatiti kukabiliana na vitendo vya uhalifu  wa aina zote na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachothibitika kuhusika na matukio ya uhalifu wa matumizi ya mabomu na tindikali.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa mara kwa moja kwa jeshi hilo iwapo watawabaini watu au kikundi chochote kinachofanya vitendo vinavyoashiria uhalifi, hasa wa mabomu na tindikali.

Akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo, Silima alisema upelelezi wa matukio hayo hauwezi kuwekwa hadharani, hasa katika hatua za awali kwa vile kufanya hivyo ni kuharibu upelelezi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru