Tuesday 3 June 2014

Bendera aongoza mamia kumzika mtoto Nasra


NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, jana aliongoza mamia ya wakazi wa mkoa huo katika mazishi ya mtoto Nasra Mvungi, aliyekaa kwenye boksi kwa miaka minne.
Nasra alifariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa amelazwa akitokea katika Hospitali ya Rufani ya Morogoro.
Mazishi hayo yalifanyika katika makaburi ya Kola,  Manispaa ya Morogoro, ambayo yalitanguliwa na ibada ya sala pamoja na kuuaga mwili wa mtoto huyo katika Uwanja vya Jamhuri, mjini hapa.
Katika salamu zake, Bendera alikemea vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wazazi, walezi na jamii kwa ujumla na kusababisha maradhi kwa watoto.
Aliwataka viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kujenga tabia ya kufutilia katika maeneo yao na kufichua vitendo hivyo mapema ili kuweza kuwachukulia hatua wahusika kabla ya madhara kutokea.
Kwa upande wake,  Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Morogoro, Ally Omari, alisema ana shaka na Uislamu kwa wahusika wa tukio hilo.
Alisema wahusika waliofanya ukatili dhidi ya mtoto huyo ni  kinyume cha sheria na maadili ya dini hiyo. Alisema Uislamu unafundisha upendo na si ukatili.
“Tendo hili linaonekana kuwa na imani za kishirikiana ndani yake. Haiwezekani mtu kumfungia mtoto ndani ya boksi huku akiwa anajisaidia humo na ukawa unaridhika na harufu,” alisema.
Naye Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Aziz Abood, alisema alipata shida kutoka kwa wabunge wenzake waliokuwa bungeni kutokana na  kitendo hicho, ambao walikuwa wakihoji kuhusiana na ukatili aliofanyiwa mtoto huyo.
Aidha, Mbunge huyo aliahidi kushirikiana na Bendera kuhakikisha sheria inachukuwa mkondo wake kwa wote waliohusika na ukatili huo. Alisema  endapo watatoka kwa njia ya panya, watarudishwa tena ndani.
Mbunge huyo aliahidi kumfanyia hitima ya mwisho mtoto huyo, ambayo itafanyika katika Uwanja wa Jamhuri.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru