Thursday 12 June 2014

Bei ya mafuta, saruji zidhibitiwe


Na mwandishi wetu
WAKATI Bajeti Kuu ya serikali ya mwaka wa fedha 2014/2015, ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, ameshauri bei ya mafuta idhibitiwe na kuwa chini.
Alisema mafuta ni nishati muhimu ambayo inagusa maisha ya kila mwananchi na kwamba yakipanda bei yanachangia maisha ya wananchi kuwa magumu.
Dk. Bana alisema hayo jana alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu muelekeo wa bajeti kuu ya serikali itakayowasilishwa bungeni mjini Dodoma.
Mbali na mafuta, Dk. Bana alishauri kuwe na bei moja ya mabati na saruji ambayo kila mwananchi ataweza kununua bidhaa hizo.
Alisema kama bizaa hizo zitakuwa na bei moja Watanzania wengi watamudu kujenga nyumba bora kwa gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Dk. Bana, kupandisha bajeti ya pombe, sigara na vinywaji vingine vyenye kemikali hakuwezi kuepukika.
Alisema mataifa mengi dunia yanapandisha bei bidhaa hizo ili kupunguza athari zitokanazo na bidhaa hizo.
Dk. Bana alisema anaiomba serikali iwabane watu wanaokwepa kulipa kodi na kwamba wakati umefika kila mtu kuwa na tabia ya kulipa kodi.
“Hata hizi bodaboda zinatakiwa zitozwe kodi, kuondoa kodi kwa bodaboda naona si sawa sawa,” alisema.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, walisema wanatumai itaboresha mfumo wa kodi na kuzuia mfumuko wa bei.
Pia, walishauri bajeti ya mwaka huu wa fedha iboreshe sekta ya elimu na itoe fursa za ajira kwa Watanzania.
Ndebile Ally alisema anategemea mishahara itapanda na kodi yake itashuka.
Norah Rugarabamu, mmiliki wa maduka ya nguo na vipodozi, alisema kwa muda mrefu wafanyabiashara wanalia na mfumo wa kodi na ushuru ambao haujapatiwa ufumbuzi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru