Monday 16 June 2014

Mwenyekiti wa zamani CHADEMA hataki siasa


Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa zamani wa CHADEMA Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Joseph Yona ambaye alijiuzulu wadhifa huo  baada ya kutekwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana mwaka jana kisha kutupwa katika ufukwe wa Ununio, ameibuka na kudai hatajihusisha na siasa tena maishani mwake.
Akizungumza na mwandishi  wa habari hizi,  jijini Dar es Salaam, Yona alisema kuwa tangu alipokumbwa na tukio hilo aliamua kubwaga manyanga ya kujihusisha na masuala ya saisa ambayo aliita ni mchezo mchafu.
“Sitaki tena kusikia kitu kinachoitwa siasa. Watu walizusha kuwa nimehamia CCM sio kweli. Nipo naendesha maisha yangu nje kabisa ya siasa. Nilinusurika kufa na sikupata msaada wowote wa maana zaidi ya kujiuguza mwenyewe,”alisema Yona.
Alieleza kuwa kilichomuuma zaidi ni kwamba baada ya kupata kipigo na kulazwa hosipitali kisha kuruhusiwa kwenda kujiuguza nyumbani  aliporejea kazini alitimuliwa.
“Nilifukuzwa kazi. Hii inaonekana ni jinsi gani hila zinavyofanyika katika siasa za Tanzania. Siwezi kuhatarisha maisha yangu wakati nina mifano hai ya mambo ya kutisha yaliyonikumba na nikaachwa nikipambana peke yangu. Sitaki kabisa kujihusisha na kitu kinachoitwa siasa na kamwe siwezi kurudi CHADEMA wala kuhamia CCM nitabaki raia wa kawaida tu ili niweze kufanya mambo yangu,” alisema Yona.
Akiwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Temeke, mwaka jana Yona alitekwa na watu wasiojulikana  katika mazingira ya kutatanisha, kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya kabla ya kutupwa katika ufukwe wa Ununio tukio ambalo  lilivuta hisia za watu hapa nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru