Tuesday 3 June 2014

Naibu Meya, Diwani watinga kizimbani


NA LILIANI JOEL,ARUSHA
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Prosper Msofe (CHADEMA) na  Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Arusha, Efata Nanyaro, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, kujibu shitaka la kudhuru mwili.
Awali, viongozi hao ambao pia ni madiwani wa Jiji la Arusha, walifikishwa katika mahakama hiyo saa 3.05 asubuhi na kukalishwa eneo maalumu, lakini ghafla waliamriwa kukabidhi vifaa vyao pamoja na fedha kwa watu wao wa karibu na kuswekwa rumande kabla ya kutinga kizimbani.
Hata hivyo, saa moja baadaye kulitokea mabadiliko kwani viongozi hao iliamriwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru-Arusha, kujibu shitaka hilo, hali iliyowafanya kupagawa.
Wakisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Mary Lucas, mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda, ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja Aprili 16, mwaka huu, eneo la Levolosi jijini Arusha, walifanya shambulio la kudhuru mwili kwa mgambo wa Jiji, William Mollel.
Mwendesha mashitaka alidai washitakiwa kwa pamoja walimpiga kifuani na sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha maumivu makali wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.
Walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana ya watu wawili ya sh. milioni moja kila mmoja na barua ya utambulisho kutoka kwa viongozi wa maeneo wanayoishi. Pia hawaruhusiwi kutoka katika mkoa wa Arusha bila kibali cha mahakama.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru