Monday 16 June 2014

Mwenge kuzindua miradi ya mamilioni wilayani Gairo


NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MIRADI saba yenye thamani ya sh. milioni 510 inatarajiwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika mbio za Mwenge wa Uhuru  wilayani Gairo mkoani Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Khanifa Karamagi alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema  Mwenge wa Uhuru utapokewa  leo katika mpaka wa Mkoa wa Morogoro na Dodoma ukitokea wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Khanifa alisem  kati ya miradi  itakayozinduliwa katika wilaya hiyo ni nyumba mbili za kuishi watumishi wa mamlaka ya mji mdogo wa Gairo  na nyumba  ya kulala wageni iliyopo katika eneo la Ukwamani  Gairo, zahanati  ya  Kijiji cha Madege na  mradi wa shamba darasa la ufugaji nyuki na hifadhi ya mazingira Kata ya Msingisi.
Kwa upande wa miradi itakayowekewa mawe ya msingi ni  zahanati katika Kijiji cha Kwipipa na  mradi wa uchimbaji kisima cha maji Kata ya Kibedya na ujenzi wa  nyumba ya mwalimu Chakwale.
Mkuu huyo wa wilaya aliwashukuru wananchi kwa kuchangia nguvu na mali zao katika maandalizi hayo  na kuwataka kujitokeza kwa wingi katika mapokezi hayo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru