Tuesday 10 June 2014

SAKATA LA CHATU


‘Mzee wa Kanisa’  aibua siri mpya

  • Amkana chatu, adai ni njama za majirani
  • Mke adai mumuwe ni msafi si mshirikina

SHAABAN MDOE NA LILIAN JOEL, ARUSHA
MFANYABIASHARA Joseph Magesa anayedaiwa kufuga nyoka aina ya Chatu nyumbani kwake, ameibua mapya kwa kudai kuwa hahusiki naye.
Pia, amedai kuwa hizo zinaweza kuwa njama za majirani zake, zilizolenga kumchafua na kwamba, suala hilo amemwachia Mungu kwani ndiye ajuaye ukweli.
Magesa, ambaye alikuwa akijitambulisha kuwa ni Mzee wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Monica, jijini hapa, alisisitiza nia yake ya kufika kanisani hapo kula kiapo kama alivyoahidi.
Hata hivyo, juzi Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Simon Tengesi, alisema hawamtambui Magesa kama ni Mzee wa Kanisa. 
Pia, alisema kanisa hilo halina utaratibu wa kuwa na viongozi hao na  vikao vinaendelea kujadili hatua ya Magesa kulihusisha katika tukio hilo kwani, ni kulichafua.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Magesa alisema hafahamu chatu huyo alipotoka na kwamba, huenda ikawa ni njama za majirani kutaka kumchafulia jina.
Alisema alipanga kufika kanisani Jumapili, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kubanwa na majukumu nje ya Arusha na kwamba, atatimiza ahadi yake ili kuudhirishia umma kuwa si mfuasi wa vitendo vya kishirikina.
Pia alisema atazungumza na waandishi wa habari ili kueleza ukweli wa mambo na baadaye atamwachia Mungu suala hilo.
“Mpaka sasa nimemkabidhi Mungu jambo hili, lakini nitafika kanisani na familia yangu kula kiapo kisha nitazungumza nanyi (waandishi),” alisema Magesa.
Aliongeza: “Huenda chatu huyo aliwekwa ama kutumwa na watu wasio na nia njema kwangu kwa lengo la kunidhuru, ila bahati nzuri hatukuwepo.”
Kuhusu kanisa kumkana, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa linaweza kuibua malumbano, lakini baadaye mambo yatabainika.
Naye mkewe Selina, akizungumza kwa simu akiwa jijini hapa, alisema ameishi na mumewe kwa miaka 10 sasa na hajawahi kusikia wala kuona vitendo vya ushirikina.
“Niko na mume wangu miaka mingi, sijawahi kusikia kuwa anafuga nyoka ndani wala sijafiwa na mtoto yeyote, wote watatu wapo ila nashangaa kusikia kauli kwamba mume wangu aliagiza nyoka asiuawe kwa kuwa ni mtoto wake ama mama yake mzazi,” alisema Selina.
Alisema watoto wake wamehojiwa na Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU) Kanda ya Kaskazini, kuhusiana na tukio hilo na kwamba, muda wote familia yake itakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru