Friday 27 June 2014

Mbaroni kwa kumbaka bintiye



NA DOROTHY CHAGULA, MUSOMA
MKAZI wa Musoma mkoani Mara, Emmanuel  Lucas, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka kwa nyakati tofauti binti yake wa miaka 19 (jina linahifadhiwa) na kumwambukiza ukimwi.
Lucas (52), anatuhumiwa kufanya kitendo hicho kuanzia mwaka 2007 na  kumsababishia binti yake kupata maambukizi ya ukimwi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Paul Kasabago, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akimbaka binti yake huyo mara kwa mara hadi kupata ujauzito, ambapo mtoto aliyezaliwa alifariki dunia.
Alisema binti huyo baada ya kujifungua, alipimwa afya yake na kugundulika kuwa ni mwathirika wa virusi vya ukimwi, hivyo kutoa taarifa  polisi mjini hapa.
Wakati huo huo, mtoto Catherine Emmanuel (4) wa kijiji cha Masinono wilayani Butiama, amepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Juni 22, mwaka huu, akiwa mikononi mwa baba yake wa kufikia, Emmanuel Dinda.
Alisema  kabla ya kupotea, mtoto huyo alisindikizwa nyumbani kwao na mtoto mwenzake Nelea Emmanuel (9), ambaye alimkabidhi kwa baba yake huyo na wakati anaondoka kurudi kwao alisikia mwenzake akiwa analia.
Kwa mujibu wa Kamanda Kasabago, Nelea alimweleza bibi yake kuwa alimwacha mwenzake analia huku mlango ukiwa umefungwa, lakini bibi yake aliichukulia kuwa hali ya kawaida kwa mtoto kuadhibiwa.
Alisema baadaye mama mzazi wa Catherine, Anastazia Emmanuel, wakati akirejea kutoka kisimani alikutana na mumewe akiwa amebeba kiroba chenye kitu kizito ndani yake akienda kusikojulikana.
Alisema mama huyo, alipofika nyumbani alikuta mwanawe hayupo, huku kukiwa na kinyesi na ndala ndani ya nyumba, ndipo alipoanza kumtafuta.
Polisi inamshikilia Dinda ili aeleze mazingira ya kupotea kwa Catherine.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru