Monday 16 June 2014

Wengi wajitokeze kuchangia damu kwa wingi- Mama Salma


Na Anna Nkinda ñ Maelezo, Kigoma
JAMII imetakiwa kujenga tabia ya kuchangia damu kwa hiari kitendo ambacho kitapunguza vifo vya kina mama wajawazito 363 vinavyotokea kila mwaka kutokana na tatizo la ukosefu wa damu wakati wa kujifungua.
Wito huo ulitolewa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, wakati akizungumza na wananchi wa Kigoma kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani humo.
Mama Salma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema takwimu zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya vizazi hai 100,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na  tatizo la uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa damu.
ìNi dhahiri vifo vinavyotokana na uzazi viko juu na kwa bahati mbaya waathirika wakubwa ni wasichana chini ya umri wa miaka 15, makundi mengine yanayohitaji kuongezewa damu ni kina mama wajawazito wakati wa mimba na kujifungua, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa ukosefu wa damu unaosababishwa na malaria kali na magonjwa mengine, ajali, wagonjwa wa saratani, upasuaji mkubwa wa moyo, anemia, seli mundu na hemophilia,” alisema.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa watu wote kuhakikisha wanatoa damu ili jamii iweze kutimiza mahitaji yake kwani kunapokuwa na akiba ya damu iliyo salama kuna kuwa na uhakika wa tiba.
Mwenyekiti wa WAMA alisema mtu yeyote mwanamke au mwanaume anaweza kuchangia damu ikiwa ana afya njema, umri kati ya miaka 18 hadi 65, uzito usiopungua kilo 50, wingi wa damu zaidi ya gramu 12 kwa desilita, kutokuwa na shinikizo la damu na kwa mwanamke asiwe mjamzito au anayenyonyesha.
Kwa upande wake,  Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,  Dk. Stephen Kebwe, alisema tangu kuanzishwa kwa mpango wa damu salama mwaka 2004 kumekuwa na ongezeko la wachangia damu kwa hiari kutoka kiasi cha chupa 5,000 kwa mwaka 2005 hadi chupa 160,000 kwa mwaka 2013.
ìChangamoto zinazoukabili mpango huu ni mahitaji makubwa kuliko upatikanaji wa damu,  inakadiriwa mahitaji ya damu kwa mwaka kitaifa ni wastani wa chupa 400,000 hadi 450,000, uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari, uuzwaji wa damu usio halali hospitalini jambo ambalo linakatisha tamaa wachangia damu wa hiari na matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali,î alisema Dk. Kebwe.
Siku ya Wachangia Damu Duniani ambayo  kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘DAMU SALAMA UHAI WA MAMA’ ni ukumbusho wa siku ya kuzaliwa kwa Karl Landsteiner, ambaye ndiye aliyegundua mfumo wa makundi ya damu A, B na O na kuzawadiwa tuzo ya Nobel.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru