Tuesday 10 June 2014

Kesi ya Madabida yaanza kuunguruma


NA MWANDISHI WETU
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), ilikagua na kugundua dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) zilizotengenezwa na Kiwanda cha Tanzania Pharmacentical Ltd (TPL), kinachomilikiwa na Ramadhani Madabida kuwa ni bandia.
Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Osward Tibabyekomya, mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba, wakati akiwasomea maelezo ya awali Madabida na wenzake.
Madabida, ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPL na wenzake, wanakabiliwa na kesi ya kuingiza na kusambaza dawa bandia za kupunguza makali ya ukimwi na kuisababishia mamlaka husika hasara ya sh. milioni 148.
Washitakiwa wengine ni wafanyakazi wa kiwanda hicho, Mkurugenzi Uendeshaji, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msoffe na Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango, pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Meneja Udhibiti Ubora, Sadick Materu na Ofisa Udhibiti Ubora, Evans Mwemezi.
Akiwasomea maelezo hayo, Tibabyekomya alidai  kiwanda cha TPL kiliingia mkataba na MSD wa kutengeneza dawa hizo na kwamba mwaka 2011, waliagizwa dawa hizo.
Alidai kati ya Aprili 5 na 11, mwaka huu, walipeleka makopo 12,252 †ya dawa bandia na kulipwa sh. milioni 148.3 kupitia hundi mbili.
Wakili huyo alidai kati ya Aprili na Mei, mwaka 2012, MSD ilisambaza dawa hizo katika vituo vyake vya kanda, hata hivyo Agosti, mwaka huo, TFDA ilipata taarifa kuna dawa hizo ambazo ni bandia hivyo  wakaagiza kila kanda ifanye ukaguzi.
Aliendelea kudai kuwa baada ya ukaguzi, waligundua dawa zilizotengenezwa na kiwanda hicho ni bandia, zina muonekeano tofauti na zilizotakiwa kutengenezwa hivyo waliamuru zirudishwe na zote zilibainika kuwa bandia.
Washitakiwa hao walikiri majina na vyeo vyao, wafanyakazi wa TPL walikiri kiwanda hicho kutengeneza dawa za ARV na waliingia mkataba na MSD, lakini walikataa kuwa dawa hizo zilikuwa bandia.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 30, mwaka huu, kwa kutajwa na itaanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri, Julai 28, mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Madabida, Shamte, Msoffe na Fatma, wanadaiwa Aprili 5 mwaka 2011, waliisambazia MSD makopo 12,252 ya dawa bandia, ikionyesha zimetengenezwa Machi, 2011 na mwisho wa matumizi Februari, mwaka jana.
Washitakiwa hao wanadaiwa kujipatia sh. milioni 148.35 kwa madai ni malipo halali ya dawa hizo.
Materu na Mwemezi wanadaiwa, kati ya Aprili 5 na 13, 2011, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa MSD, walishindwa kutumia uwezo wao wote kuzuia kutendeka kwa kosa hilo.
Washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia mamlaka husika hasara ya sh. milioni 148.3 kwa kusambaza dawa bandia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru