Wednesday 25 June 2014

Kafulila amchefua Werema



  •  Anusurika kuchapwa makonde bungeni
  •  Sitta, Wasira waingilia kati kumwokoa

NA WAANDISHI WETU, DODOMA
MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), jana alichafua hali ya hewa bungeni na kunusurika kuchapwa makonde kwa kumtolea kauli za kuudhi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Pia Kafulila ametakiwa kukabidhi ushahidi alio nao kuhusiana na malipo yaliyofanywa kwa Kampuni ya IPTL kupitia akaunti ya Escrow kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Spika wa Bunge.
Mara kadhaa Kafulila amekuwa akirusha makombora kwa baadhi ya mawaziri na watendaji, huku serikali ikitoa ufafanuzi kuhusiana na malipo hayo.
Pia imelikabidhi sakata hilo kwa CAG, TAKUKURU na mamlaka zingine kwa uchunguzi zaidi ili kubaini ukweli wake.
Hata hivyo, jana Kafulila alisimama kuomba mwongozo wa Mwenyekiti Mussa Zungu, ambapo alihoji sababu za serikali kutoa fedha hizo kuilipa IPTL.
Alisema hakuna hukumu ya mahakama yoyote ambayo iliamrisha kufanyika kwa maamuzi hayo hivyo, kutaka mwongozo ni kwanini fedha hizo zililipwa.
Mwenyekiti Zungu alimtaka Jaji Werema kutoa ufafanuzi kuhusiana na hoja ya Kafulila, ambapo alisema fedha hizo hazikuwa na serikali.
Jaji Werema alisema kumekuwa na taarifa potofu kuwa serikali imetoa fedha hizo kuilipa IPTL, jambo ambalo si la kweli na ni upotoshaji mkubwa.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakisambaza vipeperushi hata ndani ya Bunge kuhusiana na upotoshaji huo ili kuendelea kuwapotosha wananchi.
Hata hivyo, wakati Jaji Werema akiendelea kutoa ufafanuzi huo, Kafulila alianza kutoa kauli zenye kuudhi ikiwa ni pamoja na kumweleza naye (Jaji Werema) ni miongoni mwa watuhumiwa wa kashfa hiyo.
“Mmojawapo kati ya watu wanaosambaza habari hizo ni huyo anayetoa maneno machafu. Kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana kama ni suala ya ESCROW kulikuwa na ugomvi wa familia,” alisema Jaji Werema huku akionyesha kuchukizwa na kauli za Kafulila.
Alisema kama suala la wanahisa wawili wa IPTL, walitofautiana na fedha hizo si za serikali, ulizuka ugomvi kati ya wanahisa hao na mmoja kutaka IPTL ifilisiwe huku mwingine akipinga juu ya jambo hilo.
“ESCROW si fedha ya serikali, fedha ya serikali haikai kwenye akaunti hiyo, kama unataka kuleta mambo ya nje nisubiri pale nje,” alizidi kufura Jaji Werema baada ya Kafulila kurusha kijembe kingine akimtuhumiwa kuwa ni mwizi tu.
“Wanyankore wanasema tumbili hawezi kuamua kesi ya msitu, hivyo naomba nisikilize hata kama nina makosa we nisikilize kwanza,” alisema Jaji Werema na kusababisha zogo.
BUNGE LAAGIZA USHAHIDI
Kutokana na mvutano huo, Zungu aliwataka Kafulila kuwasilisha vyake TAKUKURU na kwa CAG na nakala kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Baada ya agizo hilo, Mwenyekiti Zungu aliahirisha kikao hicho, ambapo Jaji Werema huku akionekana mwenye hasira aliinuka kwenye kiti chake na kumfuata Kafulila alipo.
Hata hivyo, busara ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Stephen Wasira (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Uhusiano na Uratibu) na Dk. Asha-Rose Migiro (Waziri wa Katiba na Sheria), ilisaidia kumtuliza munkari. 
Mawaziri hao walilazimika kumzuia Jaji Werema kwenda kumvaa Kafulila, ambaye kwa wakati huo baadhi ya wabunge walikuwa wakimchukua kumtoa nje ya ukumbi.
Nje ya ukumbi hali iliendelea kuwa tete, ambapo Jaji Werema alitaka kumvaa tena Kafulila huku baadhi ya wabunge wakionekana kuwa kwenye vikundi kujadili mvutano huo.
Mnyika na madai mapya
Baada ya tukio hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitisha mkutano wa wanahabari na kueleza kuwa itawasilisha hoja binafsi kuomba uchunguzi kuhusiana na suala la malipo kwa IPTL.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, alisema pamoja na kupeleka hoja hiyo bungeni na iwapo hatua hazitachukuliwa ndani ya siku mbili, ataanza kukusanya sahihi za wabunge ili kuomba kung’olewa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru