Wednesday 25 June 2014

NHC yaahidi kufanya makubwa zaidi


NA MOHAMMED ISSA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limedhamiria kuyabadilisha maeneo ya jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine nchini baada ya kuzindua ujenzi wa miji midogo.
Limesema miradi hiyo itakapokamilika itabadilisha mandhari ya maeneo mbalimbali nchini na kuyafanya kuwa ya kisasa.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, kwenye jukwaa la uwekezaji  lililoshirikisha baadhi ya wakuu wa mikoa na wadau mbaliambali.
Mchechu alisema wataanza na ujenzi wa miradi mitatu ikiwemo ya miji midogo katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha pamoja na kuendeleza nyumba zao zilizobomolewa.
Alisema katika jiji la Dar es Salaam, watakuwa na mradi wa Salama Kigamboni na Kawe ambayo italifanya jiji hilo kubadilika na kuwa la kisasa.
Mchechu alisema katika miradi hiyo, kutajengwa nyumba nyingi za kuishi, biashara na sehemu za huduma muhimu na kwamba itakapokamilika itabadi muonekano wa maeneo hayo.
Alisema mradi mingineni utakaotekelezwa ni wa Usa River Safari City utakaojengwa Arusha na kwamba unalenga kulibadilisha jiji hilo na kuwa la kisasa.
Mchechu alisema kila mradi utagharimu dola za Marekani bilioni mbili (zaidi ya sh. bilioni 3.4) na itakamilika kati ya kipindi cha miaka saba mpaka 12.
Alisema miradi mingine ambayo itatekelezwa ni pamoja na Bagamoyo, Dodoma, Mbeya, Mtwara, Lindi, Mwanza na meneo mengine nchini.


Mchechu alisema jukwaa hilo limetokana na mkutano mkubwa wa wawekezaji waliofanya hivi karibuni nchini Dubai.
Mkurugenzi huyo alisema miradi mingine ambayo itatekelezwa katika jiji la Dar es Salaam, ni mradi wa ujenzi wa miji midogo Buguruni.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema serikali inaridhishwa na utendaji unaofanywa na NHC.
Alisema katika kipindi kifupi shirika limefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya makazi na kwamba miradi hiyo itakapokamilika itaifanya miji hiyo kuwa ya kisasa.
Profesa Anna alisema kampuni za uwekezaji kwenye sekta ya nyumba ni muhimu na hunyanyua uchumi wa nchi.
Alisema ili taifa liweze kuendelea ni lazima liwe na mipango miji na kwamba kupanga miji sio kukata viwanja bali kuna hitaji mambo mengi.
Profesa Anna aliwataka wananchi kuwa tayari katika suala la kupanga miji na maeneo yote yatakayopangwa ni lazima yafidiwe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru