Monday 16 June 2014

Vigogo wahusishwa ajali za barabarani


Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya vigogo nchini wanadaiwa kukwamisha mchakato wa kuzuia matumizi ya mabasi chakavu ya abiria, ambapo huingilia kati pindi sheria inapotaka kuchukua mkondo wake.
Pia, baadhi wamekuwa wakilazimisha askari wa usalama barabarani kutojaribu kuyakamata mabasi hayo, hatua inayodaiwa kukwamisha utendaji kazi wa askari.
Kwa mujibu wa sheria, magari yote yaliyochakaa hayaruhusiwi kubeba abiria ili kupunguza ajali ambazo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na uchakavu.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alisema watu 4,002 nchini walifariki dunia katika ajali za barabarani zilizotokea mwaka jana idadi ambayo iliongezeka ikilinganishwa na  vifo 3,969 vilivyotokea mwaka juzi.
Kamanda Mpinga alisema Mkoa wa Kipolisi Kinondoni unaongoza kwa matukio ya ajali  hizo ukifuatiwa na Ilala, Temeke, Kilimanjaro na  Pwani.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), watu milioni 1.3 wanapoteza maisha kwa mwaka kutokana na ajali za barabarani huku wengi wakipata ulemavu wa kudumu na kuwa tegemezi.
Katika kuhakikisha ajali hizo zinapungua Umoja wa Mataifa (UN) ulizitaka nchi wanachama kupunguza ajali hizo hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.
Moja ya mikakati ya serikali katika kupunguza ajali, ni kuondoa magari chakau barabarani, lakini hatua hiyo inakwamisha na baadhi ya vigogo ambao wengi ni wamiliki na wengine wana uswahiba wa karibu na wamiliki wake.
Inadaiwa kuwa baadhi ya magari  ni chakavu ambayo, yanahatarisha maisha ya abiria.
Uchunguzi uliofanywa na Uhuru ulibaini kuwa baadhi ya magari chakavu yanayobeba abiria ni mabasi yanakwenda mikoa ya kusini na baadhi ya wilaya ambazo miundombinu yake si mizuri.
Inadaiwa kuwa baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani wanaogopa kuyakamata mabasi hayo kutokana na kuhofia kupoteza ajira zao.
“Baadhi ya mabasi na malori ambayo ni chakavu na kisheria hayaruhusiwi kufanya kazi tunashindwa kuyachukulia hatua kwa sababu ya kuhofia kupoteza ajira. Tunajitahidi kufuata sheria za usalama ili kuepusha ajali na kulinda usalama wa abiria, lakini tunakwazwa kwa baadhi ya watendaji wakubwa kutuingilia kwenye kazi zetu,” alisema askari mmoja wa usalama barabarani.
Aliongeza kuwa baadhi ya mabasi yanapokamatwa wahusika huwasiliana na wamiliki wake, ambapo muda mfupi huwasiliana na viongozi wa juu wa polisi ambao hutoa maagizo ya kuachiwa kuendelea na safari.
“Mabasi mengi ni chakavu na hayastahili kubeba abiria, lakini yapo barabarani kwa nguvu za watu. Madereva wake ni wakaidi kwa sababu wamepewa maagizo ya kufanya watakalo na wanapokamatwa hupiga simu. Mara nyingi tunapotimiza majukumu yetu unasikia umepigiwa simu na kupewa amri ya kuruhusu basi kuendelea na safari,” alisema askari mwingine, ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini.
Hata hivyo, alisema wamekuwa wakiumizwa na kauli za ukali za baadhi ya viongozi na watendaji, pindi kunapotokea ajali na kusababisha maafa huku wenyewe wakiwa ndio chanzo cha tatizo.
Kwa upande wake, Ally Maftah, ambaye ni dereva wa kampuni moja inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Kilwa mkoani Lindi, alisema wanalazimika kuendesha mabasi chakavu na mabovu kutokana na ukosefu wa ajira.
Alisema kitendo cha kuendesha mabasi hayo mbali na kuhatarisha maisha ya abiria pia, maisha yao yapo hatarini kwani, ajali huwa haichagui.
Juhudi za kumpata Kamanda Mpinga, ziligonga mwamba baada ya kuambiwa kuwa yuko likizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru