Monday 30 June 2014

Watoa huduma za afya wadhibitiwe-Balozi Mchumo


NA KHADIJA MUSSA
SERIKALI imeombwa kuharakisha utaratibu wa kudhibiti gharama za huduma za afya hususan upande wa dawa ili kuwapunguzia mzigo wananchi.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya watoa huduma za afya kupandisha gharama kila kukicha, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa.
Pia, watoa huduma hao wametakiwa kuacha tabia ya kubagua wagonjwa wa kadi na kuthamini wale wanaotoa pesa taslimu.
Mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Balozi Ali Mchumo, alitoa ombi hilo jana alipokuwa akizungumza na wadau wa mfuko wa afya, mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema wakati umefika wa kudhibiti watoa huduma za afya ili kuwaondolea gharama wananchi kwani wanapata shida katika upatikanaji wa huduma hiyo, kutokana na kutokuwepo kwa mfumo wa kudhibiti gharama.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alisema ili kuweza kutatua tatizo la udanganyifu wa madai, uwepo utaratibu wa kutoa huduma kwa njia ya TEHAMA.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, aliziagiza Manispaa za mkoa wa Dar es Salaam, kuharakiasha mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu utaratibu wa Tiba kwa Kadi (TIKA).
ìUlimwenguni kote kwa sasa matumizi ya kadi katika utoaji wa huduma za kijamii ndio mtindo unaotumika, kwa bahati mbaya  hapa nchini, baadhi ya watoa huduma huthamini wagonjwa wanaotoa fedha taslimu, tabia hii lazima ikome,î alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Hamis Mdee, alisema katika mwaka ujao wa fedha, wanatarajia kuandikisha upya wanachama wao na kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ili kuweza kuwatambua wanachama wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru