Thursday 12 June 2014

Mbivu, mbichi za bajeti leo



  • Vyanzo vipya vya mapato, misamaha gumzo
  • Serikali yasikiliza mapendekezo ya wabunge
  • Kuongeza bil. 200/-, wizara kubanwa zaidi
  • Wananchi: Bei ya mafuta, saruji zidhibitiwe

NA SELINA WILSON, DODOMA
MACHO na masikio ya Watanzania leo yataelekezwa mjini Dodoma, wakati Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, atakaposoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Tayari bajeti hiyo ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa ili kutoa mwelekeo wa taifa, imeibua msuguano mkali baina ya serikali na wabunge.

Mjadala mkali kuhusu mgawanyo na uwasilishaji wa fedha za maendeleo kwenye mikoa na wilaya pamoja na misamaha ya kodi na matumizi yasiyo ya lazima kwenye wizara na taasisi za umma, umekuwa gumzo kwa siku kadhaa sasa.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema juzi kuwa misamaha ya kodi na matumizi yasiyo ya lazima kwenye wizara na taasisi za umma yatafutwa. Pia, alisema suala la ukusanyaji wa kodi za serikali litapewa msukumo mkubwa ili kuhakikisha taifa linaondokana na utegemezi.
Bajeti hiyo itawasilishwa saa 10 jioni na Saada Mkuya, ambapo matarajio ya wananchi na wabunge ni kuona serikali inakuja na majibu kuhusu vyanzo vyake vya mapato.
Mifumo ya usimamizi wa fedha, kodi na utaratibu wa utekelezaji wa bajeti ni miongoni mwa mambo ambayo serikali inasubiriwa kuyatolea ufafanuzi wa kina.
Tayari serikali imewasilisha bungeni Miswada ya Marekebisho ya Sheria Mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na nyingine ya Utawala wa Kodi, ambayo inalenga kuboresha ukusanyaji na kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa.
Kabla ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, tayari baadhi ya wabunge wameibana serikali juu ya kupanga bajeti isiyotekelezeka, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa mgawo wa fedha kutoka Hazina hadi inafikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.
Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bajeti kwa kushirikiana na serikali, iliketi kuchambua na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwenye baadhi ya maeneo ili kuhakikisha fedha zinaelekezwa kwenye masuala muhimu ya maendeleo.
Wakati kamati hiyo ikipunguza bajeti za wizara kwenye mambo yasiyo ya lazima, pia wabunge wametaka serikali ipanue wigo wa makusanyo ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea michango ya wahisani.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema jana kuwa kabla ya kusomwa bajeti hiyo, waziri mwenye dhamana na mipango, atasoma taarifa inayozungumzia mipango ya nchi kwa mwaka 2012/2015.
Spika Anne alisema kazi hiyo itafanyika baada ya kipindi cha maswali na majibu na kwamba, bajeti kuu itawasilishwa saa 10 jioni pamoja na bajeti zingine za Afrika Mashariki.
Alisema baada ya kuwasilishwa, wabunge watapata fursa ya kuijadili kwa siku tano kabla ya kupitishwa na aliwataka ambao wanataka kuchangia kujiorodhesha.
“Kwa utaratibu wa dakika saba kwa kila mchangiaji, naamini wengi mtapata nafasi, hivyo ambao hamjaomba mkajiandikishe,” alisema Spika Anne.
Viongozi mbalimbali wa Chama na serikali, taasisi za serikali na binafsi, mabalozi na viongozi wa kisiasa wanatarajiwa kushuhudia usomaji wa bajeti hiyo.

Serikali yasikiliza mapendekezo ya Bunge

Kamati ya Bajeti imeitaka Wizara ya Fedha, itafute zaidi ya sh. bilioni 200 kwa ajili ya kuongeza fedha zilizoombwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo.
Kutokana na hilo, Mwigulu amesema wizara imefanikiwa kupata kiasi hicho baada ya kupunguza katika bajeti za wizara kwa matumizi yasiyo ya lazima  ikiwemo ununuzi wa magari.
“Kama wizara tumejipanga vizuri, fedha hizo zitapatikana katika maeneo kama safari za ndani na nje,mafuta,matamasha, semina na mambo mengine yasiyo ya lazima,”alisema.
Hata hivyo, alisema fedha hizo zitatolewa na kwamba mawaziri watalazimika kutoa matokeo ya kiufanisi kulingana na  kiasi kilichotolewa.
Alisema utaratibu huo utaanza kutumika kuanzia mwaka ujao wa fedha, ambapo kabla ya bajeti ya 2015/2016, kila wizara itatakiwa kutoa taarifa juu ya matumizi ya fedha ilizoomba na matokeo.
“Kama tumetoa hela kwa ajili ya mradi wa umeme, tunataka umeme uwake , kama hakuna utekelezaji, watoe taarifa na hatua zilizochukuliwa ili kuwe na uwajibikaji,”alisema.
Mwigulu alisema kupitia utaratibu huo, pia hatua ama adhabu zilizochukuliwa, mawaziri watapaswa kuzitangaza kwa  bunge na umma.
Matarajio ya wabunge
Mbunge wa Ulanga Magharibi, Dk. Hadji Mponda, alisema serikali inatakiwa kuwa na vyanzo vipya vya mapato ikiwemo mazao ya baharini.
Alisema bila vyanzo vipya, serikali itaendelea kutegemea wahisani kwani, vyanzo vya zamani havikidhi mahitaji.
Aliyataja mazao ya baharini, kodi za nyumba za kawaida kuwa ni eneo ambalo serikali inatakiwa kulitilia mkazo kwani, kodi zake hazikusanywi kikamilifu.
“Kuna nyumba nyingi za kupanga, wamiliki wanalipwa kila mwezi ila hawalipi kodi,” alisema.
Naye Amina Makilagi (Viti Maalumu- CCM), alisema matarajio yake ni kuona serikali inakuja na bajeti ya kuwakomboa watanzania, hasa wanawake kwa kuboresha huduma za afya na maji.
Innocent Kalogeris (Morogoro Kusini- CCM), alisema serikali ijibu kiu ya nishati ya umeme ili kujenga uchumi wa wananchi wa kawaida, ambao watatumia pia nishati hiyo majumbani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru