Tuesday 10 June 2014

DCI Mgulu kuongoza timu ya makachero


NA MOHAMMED ISSA
SAKATA la wizi wa mabilioni ya fedha za wakulima wa tumbaku, limechukua sura mpya baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mgulu, kuwasili mkoani Tabora kwa ajili ya uchunguzi wa ufisadi huo.
DCI Mgulu amewasili mkoani humo, ikiwa ni siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, kutuma timu ya makachero kuwahoji vigogo wa vyama vya ushirika waliofanya ufisadi dhidi ya fedha za wakulima.
Ubadhirifu wa mabilioni hayo ya wakulima wa tumbaku uliibuliwa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliyoifanya mkoani Tabora hivi karibuni na kupokea malalamiko ya wakulima wa tumbaku.
Katika ziara hiyo, wakulima walilalamika kwa Kinana kuwa kuna ufisadi mkubwa umefanywa na viongozi wa vyama vya ushirika na kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya viongozi na watendaji wa serikali kufahamu.
Wakulima hao, walidai kuwa zaidi ya sh. bilioni 28 ambazo ni fedha zao walizokatwa kwa ajili ya ujenzi wa maghala, zimetumiwa vibaya na wajanja wachache huku majengo yaliyojengwa yakiwa chini ya kiwango.
Akizungumza kwa njia ya simu jana Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema baada ya Rais Kikwete, kutoa agizo hilo, tayari timu ya wapelelezi waliobobea kuchunguza wizi wa fedha wamewasili Tabora.
Alisema timu hiyo inaongozwa na DCI Mgulu na kwamba itafanya kazi yake kwa umakini mkubwa.
ìBaada ya agizo la Rais Kikwete, tayari timu ya wataalamu waliobobea kwenye masuala ya wizi wa fedha imeshawasili Tabora kuchunguza ubadhirifu huo wa mabilioni ya fedha za wakulima.
ìTimu hiyo iko chini ya DCI ambaye amefuata na wataalamu wenye uzoefu na uweledi mkubwa wa wizi wa fedha, tunaomba wananchi wawape ushirikiano,î alisema Advera.
Akizungumza wakati akizindua huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti katika uwanja wa Chipukizi mkoani Tabora, juzi, Rais Kikwete alisema timu ya wataalamu hao itaanza kazi jana.

MALALAMIKO YA WAKULIMA
Mwezi uliopita, akiwa ziarani wilayani Sikonge, Kinana alielezwa na wakulima wa tumbaku kuwa vigogo wa vyama vya ushirika wametafuna sh. bilioni 28 za wakulima.
Walisema pamoja na viongozi wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, kupatiwa ripoti ya ukaguzi, hakuna hatua zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kukamatwa ama kufukuzwa kazi kwa wahusika.
Naye mkuu wa mkoa wa Tabora, Fatuma Maswa, alisema asilimia 80 ya wakazi wa Tabora ni wakulima na kwamba asilimia 65 ya Tumbaku inayolimwa Tanzania inazalishwa mkoani humo.
Alisema msimu wa kilimo wa mwaka 2012-2013 mkoa ulipata mkopo wa sh. bilioni 112.6 kupitia benki za NMB na CRDB kutokana na benki hizo kuwa na dhamana ya serikali kwa ajili ya pembejeo za kilimo.
Kwa mujibu wa Fatuma, manunuzi makubwa ya sh. bilioni 90 yalifanywa na kigogo mmoja wa vyama vya ushirika bila kupitishwa na mkutano mkuu wa vyama vya ushirika.
Alisema kuna mkandarasi alilipwa sh.bilioni tatu, kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia Tumbaku na kwamba alijenga maghala mabovu na hayafai.
Fatuma alisema ukaguzi huo, ulibaini kulikua hakuna utunzaji mzuri wa vitabu vya hesabu za pembejeo na wakulima hawakupewa mbolea badala yake walikatwa sh. bilioni 1.5.
Alisema pamoja na nia njema ya serikali ya kudhamini mkopo huo, lakini kuna ubadhirifu mkubwa kwenye sekta ya Tumbaku unaosabisha wakulima kutolipwa fedha za madeni yao.
Fatuma alisema wakati umefika, serikali kuchukua hatua za makusudi za kumaliza wizi kwenye sekta ya Tumbaku unaofanywa na wajanja kwa nia ya kuwanyonya wakulima.
Alisema kutokana na ubadhirifu huo, ukaguzi uliofanywa na Ofisa Ushirika Mkuu, kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Isack Komba ndio ulibaini madudu hayo lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya waliohusika na wizi huo.
Fatuma alisema ukaguzi huo, ulibaini pembejeo hewa zenye thamani ya sh. bilioni nne, ambazo hazikuwafikia wakulima na kinachofanywa ni wizi na hata wakienda mahakamani watashinda.
Alisema baadhi ya wasambazaji wa pembejeo na wauzaji, walipewa bila kutoa huduma na kwamba pembejeo ya sh. bilioni nne haikuuzwa lakini wakulima walikatwa.
Kwa upande wake, mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, alisema taarifa ya ukaguzi ya mkoa wa Tabora imebainisha kuwa, viongozi wa vyama vya ushirika ni wezi na wanahusika na ubadhirifu huo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru