Monday 30 June 2014

TCRA yapata ubora wa kimataifa


NA RACHEL KYALA
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imepata cheti cha kiwango cha ubora kutoka Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO), kutokana na  kukidhi vigezo vya utoaji huduma kwa jamii.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa cheti hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, alisema mamlaka hiyo imepata cheti hicho kutokana na utendaji kazi wake katika kudhibiti sekta ya mawasiliano ikiwemo kujulikana kimataifa.
“Tulikwenda shule chini ya Shirika la Viwango Nchini (TBS), wafanyakazi wetu waliingia darasani na baadaye alikuja mkaguzi wa kimataifa na kukagua yale tuliyoandika ambapo tulifaulu na leo ndiyo tunakabidhiwa cheti hiki,” alisema.
Alivitaja baadhi ya vigezo vinavyozingatiwa na ISO kuwa ni pamoja jinsi wanavyowashirikisha kila siku wafanyakazi wake katika utawala  wa mamlaka, namna wanavyotumia rasilimali watu katika kufanikisha utendaji mzuri wa kazi ndani na nje ya mamlaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Maabara ya Vifaa wa TBS, Salvatory Rusimbi, alisema kigezo muhimu kinachotazamwa ni kuangalia iwapo wateja wanaridhika na huduma zinazotolewa na kampuni na taasisi zinazosimamiwa na mamlaka husika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru