Tuesday 10 June 2014

Bajeti mpya balaa



  • Serikali yatangazia kiama wakwepa kodi
  • Watakaopewa misamaha sasa kutangazwa 
  • Vikao vya chai marufuku, maendeleo kwanza 

NA SELINA WILSON, DODOMA
SIKU chache kabla ya kusomwa kwa bajeti ya serikali bungeni, wafanyabiashara na vigogo wanaokwepa kodi kwa kujificha kwenye mwamvuli wa misahama hawako salama, imeelezwa.
Hatua hiyo imetokana na serikali kuonya kuwa, haitawaogpa wala kuwaonea haya wakwepa kodi na kwamba, kuanzia sasa misamaha yote itawekwa hadharani.

Pia, imesema kuwa kila msamaha utakaotolewa na serikali utatakiwa kuendana na huduma za kijamii zilizolengwa na kuwa itawekwa kwa kufuata utaratibu wa kisheria na si kiholela.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema hayo alipozungumza kuhusu mwelekeo wa bajeti na jinsi serikali ilivyojipanga katika kusimamia makusanyo ya ndani.
"Tutafuatilia kikamilifu kwa kuwa wapo watu wanaingiza bidhaa wanapewa msamaha, lakini ukija kwenye huduma za jamii unakuta bidhaa hizo zinauzwa kibiashara,î alisema.
Alisema jambo kubwa ni ushirikiano wa wananchi na alishawaeleza mawakala wa forodha kwamba popote wanapopata taarifa za mtu kukwepa kodi ama mtu kudanganya kuhusu bidhaa ikiwa ni pamoja na kupitisha bidhaa tofauti na iliyopewa msamaha, atoe taarifa kuwa kuwa ni hujuma.
"Bahati nzuri niliyonayo, sikuzaliwa na chembe ya woga, kwa hiyo kwenye hili hakuna mkubwa wala mdogo, hakuna mtu atagusa fedha ya umma kwa kukwepa au kwa kutumia vibaya kodi ambayo ilishakusanywa halafu akapona asiguswe,î alisema.
Alisema katika eneo hilo wanahitaji ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa wananchi wakiwemo mawakala wa forodha ili kudhibiti udanganyifu kwa kuwa wapo watu wanaonyesha nyaraka zikionyesha anaingiza, lakini anaingiza vitu vingine.
Kwa upande wa misamaha ya kodi, Mwigulu alisema serikali imelenga kuziba mianya ya wa kwepa kodi kwa kupunguza au kuondoa kabisa misamaha ya kodi.
ìTumeshuhudia nchi ikitegemea zaidi wafanyabiashara wadogo na wafanyakazi kisa hawana mwanya wa kukwepa kodi, wakati wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakikwepa.
ìTutadhibiti ukwepaji kodi ili kuwapunguzia mzigo  hawa wadogo, ambao hawana namna kukwepa na wafanyakazi kuwapunguzia kodi kwenye kipato chao ili kuwapunguzia mzigo na gharama za maisha,î alisema.

MAENEO MUHIMU YA USIMAMIZI
Alisema katika Bajeti ya Serikali ya 2014/2015 yapo mambo ya msingi matano, ambayo yatasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa tofauti na zilizopita.
Mbali na kuondoa misamaha ya kodi, pia makusanyo ya ndani yatatiliwa mkazo zaidi ili kujenga uwezo wa kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea wahisani.
ìKujitegemea kuna heshima yake. Tunawaomba wabunge na wananchi watuunge mkono katika hili kwa kuwa mategemeo ya misaada yameendelea kupungua kila mwaka,î alisema.
La tatu ni kuhakikisha wanapeleka fedha kwenye mahitaji muhimu na kwa wakati ili kuhakikisha fedha za maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema uzoefu wa mwaka huu wa fedha yaani 2013/2014 unaonyesha mpaka inafikia kupitisha bajeti ya mwaka mwingine , fedha za maendeleo zilizotolewa hazijafikia malengo.

Vikao vya chai marufuku
Katika kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, Mwigulu alisema fedha zitapelekwa kwenye mambo muhimu.
ìKama hali ngumu na wananchi wanalazimika kula mlo mmoja kwa siku, walioko ofisini pia wanaweza kukosa chai ili kuwezesha mambo mengine muhimu yafanyike kwa wakati.
Tunachotaka wizara zibane matumizi tubaki na yale yenye umuhimu. Tunaomba wenzetu kwenye wizara watuunge mkono ili kuhakikisha bajeti hii inakwenda na wakati kwa maana ya mgawo wa fedha badala ya kuchelewa kama ilivyo sasa,î alisema.
Mwigulu alisema jambo lingine la nne litakalozingatiwa ni usimamizi wa fedha zinazopatikana kwani pamoja na makusanyo kidogo, lakini pia kuna uvujaji.
ìTunataka fedha inayopatikana na kupangiwa kazi fulani itumike kwa shughuli iliypokusudiwa kama. Tutahakikisha tunasimamia na kudhibiti matumizi yake,î alisema.
Alisema lengo ni kuhakikisha matumizi yaendane na thamani kwa uhalisia wa jambo
Naibu Waziri huyo wa fedha alisema eneo la tano ambalo litaangaliwa ni eneo la fedha ambazo hazitokani na kodi bali zinachangwa na wananchi na wadau wengine katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema eneo hilo ni muhimu mbalo serikali inaona kuna haja ya kulisimamia vizuri ili kuhakikisha fedha za wa wananchi zinatumika vizuri.
ìKuna wakati wananchi wanachanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa zanahanati au jengo la ofisi. Wakati mwingine fedha zao zinakuwa nyingi kuliko zinazotolewa na serikali.
ìUnakuta wananchi wamejenga jengo baadae anakuja mhandisi anasema ujenzi wake haukufutwa vigezo hivyo livunjwe. Hili litaangalia haiwezekani fedha za wananchi zikapotea bure ndio maana tumeweka kipaumbele katika eneo hili,î alisema.
Alisema upotevu wa fedha ni upotevu, hivyo serikali itakuwa makini katika fedha za umma zinachangwa na wananchi katika miradi ya maendeleo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru