Tuesday 10 June 2014

Wasafiri reli ya kati wakwama


NA RABIA BAKARI
MAMIA ya wasafiri waliokuwa wanaelekea mikoa ya kati na treni ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL),wamekwama baada ya safari hizo kuahirishwa ghafla.
Treni hiyo ambayo ilianza safari wiki iliyopita baada ya kusimama kufanya kazi kwa  miezi kadhaa, jana iliendelea kuwa kitendawili baada ya kusitisha ghafla safari hizo bila  abiria kutangaziwa  mapema. 
Wiki iliyopita, TRL  ilitoa tangazo la kuanza safari za treni ya abiria zilizosimama kutokana na reli kuharibiwa na mafuriko, na kueleza kwamba imefanyiwa ukarabati mkubwa na hivyo kuleta matumaini ya kuimarika kwa safari hizo. 
Meneja Mkuu wa Usafirishaji wa TRL, Lowland Simtengu, alinukuliwa akisema safari hizo zinaanza baada ya kukamilika kwa ukarabati wa miundombinu ya reli eneo la kati ya stesheni za Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma na kwamba hali ya miundombinu ni nzuri na wamejiandaa kikamlifu kutoa huduma ya usafirishaji.
Lakini kinyume na kauli hiyo, jana ilikuwa  shubiri kwa abiria, ambao walikuwa waondoke na treni ya saa 12:00 jioni, ambapo walipofika stesheni, walipewa taarifa za kuahirishwa kwa  safari hiyo.
Uhuru lilishuhudia abiria wakiendelea kumiminika kuingia stesheni bila kuwa na taarifa ya kutokuwepo kwa safari hiyo.
Akizungumza na  gazeti hili, Meshack Kyeke, alisema yeye si abiria, bali alikuwa amemsindikiza mkewe anayesafiri kwenda mkoani Tabora.
“Ingekuwa  ustaarabu kwa mamlaka husika kuandaa usafiri mbadala kutokana na dharura iliyokuwepo,lakini si kusubiri watu wamefika kisha kuwaambia safari hakuna,”alisema.
Kwa upande wake, Mariam Salum  alisema kutokana na kuwa na uhakika wa safari, wengi wao walifanya manunuzi ya vitu vingi, hivyo kwarudisha nyumbani ni usumbufu usiovumilika.
Abiria wengi waliotoa maoni yao, walisema ni vyema serikali ikahakikisha usafiri wa ndege na treni si wa ubabaishaji kwa vile ndivyo ilivyo katika maeneo mengi duniani.
Wakiwa na nyuso za huzuni, wengine walidai hawana pa kwenda kwa kuwa wametoka Zanzibar wakijua watapiliza moja kwa moja na hivyo watalala hapohapo stesheni.
“Tuna watoto wadogo, wagonjwa na kama haitoshi, tunatoka maeneo ya mbali, mtu umejichanga, umetafuta usafiri wa kukufikisha hapa, halafu  unafika unaambiwa hakuna usafiri, fedha inazidi kuteketea na usumbufu  wake  hauelezeki,” alisema Shabani Mlingila.
Msururu wa abiria ulipanga foleni katika dirisha la kukatia tiketi kwa ajili ya kurudishiwa fedha za nauli walizotoa kwa  ajili ya safari hiyo.
Hata hivyo, uongozi waTRL ulipata kigugumizi  cha kueleza lini safari hizo zitaanza tena, ili kuwapa matumaini abiria waliopanga kupiga kambi stesheni.
Msemaji wa TRL, Midladjy Maez, alisema chanzo cha kusitishwa kwa safari hizo ni ubovu wa reli katika eneo la Mto la Ruvu mkoani Pwani. 
Maez hakuweka wazi ni lini safari hizo zitaanza tena, badala yake aliomba aachwe kwa kuwa alikuwa akiandaa taarifa  kwa vyombo vya habari.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru