Monday 16 June 2014

Maofisa wa JWTZ, Polisi wafa ajalini


Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
OFISA WA Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Edward Mosi na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Johnson Zakaria, wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea kijiji cha Chamakweza mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 7.15, mchana.
Alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T. 164 AUS na T. 498 AZ aina ya Scania.
Matei alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Hassan Shabani mkazi wa Dar es Salaam ambapo liligongana uso kwa uso na gari dogo lenye namba za usajili Z 190 DR aina ya Isuzu Carry iliyokuwa ikiendeshwa na Meja Mosi wa JWTZ kikosi cha Kinonko, aliyekuwa akitokea Morogoro.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, katika ajali hiyo, Mkaguzi  Msaidizi wa Polisi wilaya ya Korogwe, Tanga, Zakaria alifariki dunia papo hapo.
Matei aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Yona Zakaria na Johnson  Zakaria ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufani Tumbi.
Alisema polisi wanamtafuta dereva wa Scania, Hassan Shabani, kwani alitoroka muda mfupi baada ya kusababisha ajali hiyo. Matei alisema chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru