Wednesday 25 June 2014

Arfi awageuka wapinzani


NA RASHID ZAHOR, DODOMA
MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA), juzi aliishangaza kambi ya upinzani bungeni baada ya kupiga kura ya kuunga mkono Bajeti ya Serikali, kwa mwaka wa fedha 2014/ 2015.
Arfi, ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, alikuwa mmoja wa wabunge wanne wa upinzani waliopiga kura ya kuunga mkono bajeti hiyo na kushangiliwa kwa nguvu na wabunge wa CCM.
Wabunge wengine wa upinzani waliopiga kura ya kupitisha bajeti hiyo ni John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF) na Augustino Mrema (Vunjo-TLP).
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Cheyo, Mrema na Hamad kuunga mkono bajeti ya serikali. Wabunge hao pia walifanya hivyo wakati wa kupitisha bajeti ya mwaka 2013/2014.
Kitendo cha Arfi kupiga kura ya kupitisha bajeti hiyo, kilipokewa kwa mshangao mkubwa kwa vile haijawahi kutokea kwa mbunge wa CHADEMA kufanya hivyo.
Wabunge 300 walipiga kura kwa kutamka ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’. Wabunge waliopiga kura ya Ndiyo walikuwa 234 wakati waliopiga kura ya Hapana walikuwa 66. 
Wabunge 54 hawakuwepo bungeni. Idadi kamili ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 357.
Upigaji huo wa kura uliingia dosari ilipofika saa 1.20 usiku baada ya umeme kuzimika ghafla bungeni baada ya jina la Richard Ndassa (Sumve-CCM) kutajwa. 
Kukatika huko kwa umeme kulizusha taharuki miongoni mwa wabunge na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Kutokana na giza kutanda bungeni, baadhi ya wabunge walianza kutamka maneno ya kutaniana huku wengine wakimtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aeleze sababu za kutokea kwa hali hiyo. 
Wabunge wengine walikwenda mbali zaidi kwa kuhoji kwa nini majenereta yaliyoko bungeni yalishindwa kufanya kazi, hatua iliyomfanya Spika Anne asimame na kutoa ufafanuzi kuwa tatizo lililojitokeza la kukatika kwa umeme halikutokea bungeni pekee, bali ni nchi nzima.
Alisema, kwa mujibu wa taarifa alizozipata, umeme ulikatika nchi nzima baada ya kutokea hitilafu katika Bwawa la Mtera na kwamba hata majenereta ya bunge yalipata hitilafu kutokana na tatizo hilo.
Baada ya umeme kurudi bungeni saa 1:57 usiku, upigaji kura uliendelea na kumalizika na wakati matokeo ya kura hizo yakisubiriwa, Spika Anne alimuomba Profesa Muhongo awaeleze wabunge kilichotokea.
Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuwaomba radhi wabunge na wananchi kutokana na tatizo hilo lililoikumba nchi nzima na kuongeza kuwa, lilitokana na hitilafu iliyotokea kwenye Bwala la Mtera na kuathiri vyanzo vingine vya umeme nchini.
Muhongo alitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutoa taarifa ya kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kukatika huko kwa umeme kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru