Saturday 7 June 2014

CHATU KUKUTWA KWA MZEE WA KANISA....


SHAABAN MDOE NA LILIAN JOEL, ARUSHA
SAKATA la kukutwa kwa myoka aina ya chatu ndani ya nyumba ya mzee wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha Parokia ya Mtakatifu Monica, Joseph Magesa, limechukua sura mpya baada ya Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Kaskazini kuanza uchunguzi ili kubaini iwapo kama alikuwa akimilikiwa kihalali.
Akizungumza na UUHURU WIKENDI ofisini kwake jana, Kamanda wa kikosi hicho, Paschal Mrina, alisema uchunguzi huo umeanza mara moja, muda mfupi baada ya kupokea simu kutoka kwa wasamaria wema kuhusu kuonekana kwa chatu huyo ambapo alituma maofisa wake.
Awali, baada ya kupokea simu hiyo alidhani chatu huyo alikua ni wa porini ambaye alifika katika makazi ya watu, lakini baada ya maofisa wake kufika eneo la tukio, walikuta chatu huyo ameshauawa na kwamba alitokea nyumbani kwa mzee huyo wa kanisa aliyekua akimfuga.
Mrina aliongeza kuwa baada ya mmiliki wa nyumba hiyo kurejea kutoka safarini Dodoma, watamhoji katika mambo makuu matatu ikiwemo kufahamu iwapo alikuwa akimmiliki chatu huyo kihalali na iwapo hakummiliki kihalali atachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, Mrina alifafanua kuwa hata kama mmiliki wa nyumba hiyo alikuwa na kibali kamwe hakimruhusu kufuga na kuishi na chatu ndani ya nyumba anayoishi binadamu bali alipaswa kumfuga kwenye shamba la wanyama kama inavyofanyika kwa wanyama wengine.
ìSisi tulipokea simu kutoka kwa wananchi waliokuwepo pale tukadhani ni chatu wa porini tu, lakini maofisa wangu walipofika walikuta ameshauawa...tunachokifanya sasa tunataka kumhoji ili kufahamu iwapo alimmiliki chatu huyo kihalali na kama sivyo tutamchukulia hatua, haiwezekani kuishi ndani ya nyumba na chatu,îalisema Mrina.
WAUMINI WA KANISA WAZUNGUMZA
Wakizungumzia tukio hilo kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya waumini waliokuwa wakisali na mzee huyo wa kanisa walisema wameshtushwa na tukio hilo la muumini mwenzao kuishi na chatu ndani ya nyumba wanayemdhani alikuwa akimtumia kishirikina wakati yeye alionekana kuwa mkristo safi.
Hata hivyo, walienda mbali na kudai watautaka uongozi wa kanisa hilo kumchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kumtenga hadi pale ukweli utakapobainika kwa yeye kukiri na hata kuungama mbele ya madhabahu.
Hata hivyo, waliongeza kuwa hatua hizo za kumtenga ni pamoja na kusitisha ibada za jumuia za kila wiki zilizokuwa zikifanyika nyumbani hapo kwa waumini kwenda kusali kwa kuwa wanaamini hakuna chochote walichokipata kwa ibada hizo bali kuchuma dhambi.
WAGANGA WA KIENYEJI WAZUNGUMZA.
Mmoja wa waganga wa tiba za asili aliyegoma kutaja jina lake akizungumzia tukio hilo alidai kuwa kwa kawaida ukiona tukio kama hilo limetokea ni wazi kuwa mmiliki wa nyoka huyo alipaswa kutoa kafara kama alivyoahidi, lakini kinachoonekana alichelewa kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa chatu au mnyama yeyote aliyewekwa ndani kwa imani za kishirikina kamwe hawezi kutoka nje hivi hivi bali kuna masharti yaliyokiukwa likiwemo hilo la kutoa kafara.
Juzi, umati mkubwa wa wakazi wa jiji la Arusha na viunga vyake kuanzia asubuhi walikuwa wakifurika nyumbani kwa mzee huyo wa kanisa na mfadhili kumshuhudia chatu  huyo aliyekadiriwa kuwa na urefu wa mita nne aliyedaiwa kufugwa ndani ya nyumba ya mzee huyo.
Chatu huyo alikuwa amefungwa vitambaa vya aina mbili shingoni vya rangi nyeusi na nyeupe vikiwa na maandishi yasiyofahamika na alidaiwa kuzua tafrani ndani ya nyumba hiyo na kumkimbiza mtoto wa marehemu dada yake na mmiliki wa nyumba, kabla ya kuvunja kioo cha sebuleni na kutokea dirishani.
TABIA ZA CHATU
Nyoka aina ya chatu ndiye pekee mwenye kuweza kufugwa na kufanya urafiki na binadamu kwa sababu hana sumu ya aina yoyote, lakini ana uwezo mkubwa wa kukaba.
Baadhi ya vikundi cha sanaa na utamaduni vimekuwa vikitumia chatu kufanya sanaa za maonyesho kwa kucheza naye, kumkumbatia, kumweka kinywani na kumzungusha shingoni.
Chatu huweza kuwa rafiki wa binadamu kama ilivyo kwa mbwa au paka baada ya kuishi naye kwa muda mrefu.
Kumfuga chatu sio kazi nyepesi, bali inahitaji fedha, ujuzi, ulinzi na ukaribu ambapo mlo wake kwa siku ni wastani wa sungura watatu. Tabia nyingine ya chatu ni kuwa hula wanyama hai tu. Chatu wa kufuga hupendelea mbuzi hai, kuku au ndama.
Chatu wa kufugwa, kuna wakati huweza kutoroka na kusababisha madhara kwa watu wengine, lakini baada ya kukaa kwa muda nje huwa na tabia ya kurudi sehemu wanayofugiwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru