Monday 16 June 2014

Nape: CHADEMA wanatumia UKAWA kuficha migogoro


Na Bashir Nkoromo
KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amefichua siri ya viongozi wa juu wa CHADEMA kujificha nyuma ya kivuli cha Kundi la Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Amesema CHADEMA kinakabiliwa na migogoro mizito inayotokana na uchu wa madaraka na kwamba hatua ya kukumbatia UKAWA ni kuwapumbaza wanachama wake.
Alisema sio kweli kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, wana nia na dhamira ya dhati ya muungano huo ili kusaidia wananchi bali ni kujaribu kupoza makali ya wanachama wake wenye hasira ya kuburuzwa.
“CHADEMA wapo katika mgogoro mkubwa kutokana na baadhi ya viongozi wake hasa wa ngazi za juu kukiendesha kwa misingi ya ubaguzi... na ndiyo sababu leo au hata kesho, Mbowe hawezi kuitisha kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, na akijaribu kufanya hivyo anatimuliwa,” alisema Nape.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Jimbo la Ubungo juzi jioni, Nape alimpasha mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika kuwa akae mkao wa kuondoka kwa kuwa kodi yake ya pango inafikia ukingoni.
Alisema Mnyika aliwahadaa wananchi wakampigia kura wakiamini atakuwa mtetezi wa kweli, lakini hana analolifanya zaidi ya kuandamana.
“Mnyika tunawambia kodi yake ya pango inamalizika rasmi mwaka 2014 na hatuna mpango wa kumuongezea muda, ajiandae tu kuondoka taratibu,” alisema Nape.
Alisema, Mnyika kama walivyo wabunge katika maeneo ambako wananchi walijaribu kuwachagua wapinzani, anachofanya yeye na chama chake ni kupambana na kujenga misingi ya chama chao kuendelea kuishi na kamwe hawashughulikii matatizo ya wananchi.
“Na hili niliwaambia miaka mingi iliyopita, nilisema hapa Ubungo mkimchagua mpinzani kazi yake itakuwa kutafuta njia za kuimarisha chama chake na kamwe hataweza kujihusisha na masuala ya maendeleo yenu,” alisema Nape na kuongeza: “Mnyika kama kweli una lengo la kuwatumikia wananchi wa Ubungo, umefika wakati wa kuacha sasa na mambo ya kudai kila mara hoja binafsi bungeni, sasa udai na hoja za wananchi, maana ukiendelea kudai hoja binafsi za wananchi utadai lini?”
Alisema ni kutokana na wapinzani akiwemo Mnyika na chama CHADEMA kutokwa mapovu midomoni kila kona ya nchi wakihangaika na Katiba mpya, tena wanachozungumzia zaidi serikalikali tatu na kusingizia kwamba ndiyo mahitaji ya wananchi huku wakijua wazi kwamba wanachohitaji wananchi kama wa Ubungo ni maji, elimu na afya na siyo idadi ya serikali.
Nape alisema hivi sasa wananchi wameshastukia vyama vya upinzani kwamba vipo kwa maslahi ya wachache ni si ya wananchi kama vinavyovyojinadi.
Alisema, miongoni mwa dalili za wananchi kuvistukia vyama vya upinzani ni hali ilivyojitokeza wakati wa ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alizofanya akiambatana naye mikoani.
Nape alisema katika ziara hizo hadi sasa wanachama 12, 430 walijiunga CCM huku karibu nusu yao wakiwa wametoka katika vyama vya upinzani vikiwemo CHADEMA na CUF.
Katika mkutano huo ulioandaliliwa na Jumuia ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Nape alipokea wanachama wapya 480, wengi wao wakiwa wamehamia CCM kutoka katika CHADEMA na CUF kwa nyakati tofauti.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru