Monday 16 June 2014

MVUTANO BAJETI



  •  Kamati ya Bunge yasema serikali haitaki kusikiliza ushauri
  •  Yadaiwa haiumizi kichwa kusaka vyanzo vingine vya mapato
  •  Yabanwa na kutakiwa kurejesha mikopo ya mifuko ya hifadhi

NA WAANDISHI WETU, DODOMA
UCHAMBUZI wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015 uneonyesha kuwa mzigo wa matumizi ni mkubwa ikilinganishwa na vyanzo vya mapato.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Andrew Chenge, alipokua akiwasilisha taarifa ya kamati yake bungeni.
Chenge alisema serikali imekosa ubunifu na haitaki kupokea ushauri wa kamati kuhusiana na vyanzo vipya vya mapato.
Alisema hali hiyo imeifanya serikali kuja na vyanzo vile vile vya kitamaduni vilivyozoeleka wakati kuna vyanzo vingine vingi.
Mwenyekiti huyo alisema vyanzo hivyo vipya ni pamoja na vile ambavyo vimependekezwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaoendelea.
Vingine ni pamoja na maabara ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Chenge alisema kamati inaendelea kuishauri serikali kufanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa ili kupunguza nakisi ya bajeti na mzigo kwa walipa kodi.
Aidha kamati hiyo imesema uchambuzi huo umebaini madeni makubwa wa serikali katika bajeti ya mwaka 2013/2014.
Chenge alitolea mfano Wizara ya Ujenzi ambayo imekuwa ikitekeleza miradi ya ujenzi wa barabara bila kuwalipa makandarasi kwa wakati.
Alisema hali hiyo imeifanya wizara hiyo ikianza kila mwaka wa fedha kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni.
Mwenyekiti huyo alisema hali hiyo imeifanya wizara hiyo kutumia bajeti yake ya mwaka unaofuata kulipia madeni ya mwaka uliopita badala ya kutekeleza  iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha husika.
Pia, imeshauriwa  kuanzisha utaratibu wa  kukopa au kuazima  fedha toka vyanzo mbalimbali nafuu za kutekeleza  bajeti ya serikali badala ya kusubiri kukusanya mapato kwanza ndiyo isambaze kwa utekelezaji.
Chenge alisema utaratibu wa sasa ambao umetumika kwa muda mrefu wa kukusanya mapato kwanza ndipo matumizi yafanyike,  huchelewesha utekelezaji wa miradi na bajeti husika.
Alisema ni vyema utaratibu huo ukabidilishwa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2014/2015.
ìNi vyema sasa serikali katika bajeti ya mwaka huu wa fedha ikakopa  kutoka vyanzo mbalimbali nafuu kiasi cha kufikia angalau robo moja yaani sh, trillion tano ya bajeti ya mwaka, utaratibu huo huitwa ëcapital badgetí badala ya ‘cash budget,íí alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuna kila umuhimu wa kuharakishwa kuletwa bungeni kwa Sheria ya Bajeti itakayofanya kazi sambamba na Sheria ya Manunuzi ili kudhibiti matumizi mabaya kinyume na sheria na kanuni kwa nia ya kuweka nidhamu katika kutekeleza bajeti ya serikali.
Kwa upande wa ukuaji wa uchumi,  Chenge alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 ni wa kuridhisha na umekuwa kwa wastani wa asilimia 6.8.
Alisema katika mwaka 2013 pato halisi la taifa  lilikuwa kwa kiwango cha asilimia 7 ikilinganishwa na ukuaji wa kiwango cha asilimia 6.9 kwa mwaka 2012, asilimia 6.4 kwa mwaka 2011 na asilimia 7 kwa mwaka  2010.
Kwa mujibu wa Chenge, ukuaji wa pato la taifa kwa mwaka 2013 ulichangiwa zaidi na sekta ya mawasiliano asilimia 22.8 huduma za fedha asilimia 12.2, viwanda na ujenzi asilimia 8.6 biashara asilimia 8.3.
Hata hivyo,  alisema pamoja na kukua kwa uchumi umasikini miongoni mwa wananchi haupungui kwa kasi ya ukuaji wa uchumi huo.
Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa sekta zinazobeba na kugusa maisha ya watu wasiopungua asilimia 75 ya Watanzania wote yaani kilimo, mifugo na uvuvi hazikui kwa kasi inayotakiwa.
Alisema hiyo inatokana na serikali kutowekeza vya kutosha katika sekta hizo na kuwepo kwa muingiliano hafifu kati ya sekta zinazokua haraka na zile zinazokua polepole, pia utekelezaji usio endelevu wa sera na programu li zinzowekwa na serikali kama vile kilimo kwanza na ASDP.
Akizungumzia deni la taifa,  Chenge alisema deni hilo ni mzigo mkubwa kwa taifa na hadi sasa ni tishio kwa utengamavu wa uchumi.
Alisema kamati yake inaona shaka kuhusiana na deni hilo kutokuwa stamilivu kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa madai mengi ya ndani ambayo hayajajumuishwa katika deni la taifa na taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa madai hayo yanaendelea kuongezeka.
Alisema deni hilo limeongezeka kutoka asilimia 0.5 ya pato la taifa mwaka 2012 hadi asilimia moja ya pato la taifa mwaka 2013.
Chenge aliongeza kuwa sababu nyingine ni uwiano uliopo wa deni la taifa  na pato la taifa kiuchumi sio wa kuridhisha na ukubwa wa deni hilo hauwiani na kiwango cha uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa sasa wa asilimia saba.
Alisema taarifa zinaonyesha kuwa malimbikizo ya madai hayo hadi Desemba mwaka jana yalikuwa yamefikia sh. trillion 2.09 ambayo ni asilimia nne ya pato la taifa
YABANWA KUREJESHA MIKOPO YA MIFUKO YA HIFADHI
Serikali imeshauriwa kurejesha kwa wakati fedha za mikopo inazokopa kutoka katika mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii.
Imeelezwa kuwa kiasi cha fedha kinachorejeshwa na serikali kwa sasa ni kidogo na kwamba kutorejeshwa fedha hizo kwa wakati, kunaweza kusababisha mifuko kushindwa kulipa pensheni kwa wanachama wake watakaokuwa wamestaafu kwa kiwango wanachostahili.
Chenge alisema bungeni jana kuwa, hadi kufikia Juni 30, 2013, mifuko hiyo ilikuwa ikiidai serikali zaidi ya sh. trilioni tatu, hivyo kamati inaihimiza serikali kuweka utaratibu endelevu wa kulipa madeni hayo.
Alisema kwa upande wa mfuko wa PSPF, serikali inadaiwa sh. trilioni 3.3, ikiwa ni malimbikizo ya pensheni ya wanachama wake hadi kufikia Juni 1999.
ìSerikali imekuwa ikilipa sh. bilioni 50 kila mwaka, kiasi ambacho ni kidogo sana ikilinganishwa na kiasi inachodaiwa,îalisema Chenge na kuwa: ìKamati inaishauri serikali itumie utaratibu wa malipo kwa fedha taslim na hati fungani ili kuokoa mifuko na hatari ya kufilisika.î
Pia, kamati imeishauri serikali kuongeza kiwango cha michango yake kwa watumishi wa serikali kufikia asilimia 20 ili kufanya jumla ya mchango wa wanachama kuwa asilimia 25 ya mshahara wake.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru