Saturday 7 June 2014

Watakaochakachua mbolea kutozwa faini sh. mil. 500


NA SELINA WILSON,DODOMA
SERIKALI inakusudia kuongeza viwango vya adhabu ya faini kwa watakaochakachua mbolea kwa kuwatoza faini ya kati ya sh. milioni 100 na sh. milioni 500.
Pamoja na faini hiyo, mbolea itakayobainika kuchakuliwa na kuwa chini ya kiwango itateketezwa baada ya wakaguzi kuthibitisha kwamba imechakachuliwa.
Hayo yamo katika muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mbolea sura namba 378  uliowasilishwa bungeni Jumatano wiki hii na kusomwa kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa muswada huo, viwango hivyo vya adhabu vitasaidia kuwatia hofu ya uchafuzi na uchakachuaji wa mbolea na kuuza mbolea zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.
Katika muswada huo imependekezwa kuongeza kifungu kipya cha 40 A ambacho kitaipa Mamalaka ya Udhibiti wa Mbegu, uwezo wa kutoza faini za papo kwa hapo kwa watakaokiri makosa chini ya sheria hiyo.
Pia, imependekezwa kuongeza kifungu kipya cha 34 A ambacho kitawpa wakaguzi wa mbolea mamlaka ya kukamata  na kuteketeza mbole zilizo chini ya kiwango kilichowekwa kisheria.
ìKifungu kidogo cha (2) na kifungu hiki kinabainishwa  mambo ya msingi ambayo mkaguzi wa mbolea anapaswa kuzingatia kabla ya kuharibu mbolea iliyobainika kuwa chini ya kiwango,îilieleza sehemu ya muswada huo.
Katika muswada, inapendekezwa kifungu cha 36 kifanyiwe marekebisho ili kufuta kifungu kidogo cha (3) ambacho kinamtaka Waziri anayesimamia masuala ya mbolea kushirikiana na Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbegu katika kufanya uamuzi wa rufani zitakazowasilishwa kwake.
Kwa mujibu wa marekebisho yanayopendekezwa katika kifungu kipya cha 37 uamuzi wa rufani zote utafanywa na Waziri bila kuishirikisha bodi hiyo.
Marekebisho hayo yanayopendekezwa katika sheria hiyo yatasaidia kukuza na kuimarisha  sekata ya kilimo nchini na kuongeza ubora wa mazao ili kufikia shabaha ya nchi  juu ya mchakato wa mageuzi ya kilimo.
Kulingana na muswada huo, pia marekebisho hayo yamelenga kuwezesha utekelezaji mzuri wa jitihada za serikali juu ya sera ya Kilimo Kwanza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru