Wednesday 25 June 2014

Wajumbe CUF wagomea mapendekezo ya Seif


NA RABIA BAKARI
ZAIDI ya asilimia 85 ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu  wa CUF, wamekataa pendekezo la kutaka kuongezwa madaraka kwa upande wa mikoa.
Pendekezo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu aliyejiuzulu kupisha uchaguzi uliofanyika jana, Maalim Seif Shariff Hamad, lilikataliwa na wajumbe hao kwa madai itakuwa mzigo mzito kwa  chama.
Kutokana na hali hiyo, CUF haitakuwa na muundo unaofanana na vyama vingine ikiwemo CHADEMA na NCCR-Mageuzi, ambavyo vyenyewe vina uongozi kwa ngazi ya mkoa, na hivyo kudaiwa kuleta shida katika vikao vya pamoja.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema kutokana na utata huo, wajumbe wanaliachia Baraza Kuu la Uongozi, kuamua ni namna gani wanaweza kushirikiana katika uongozi bila kuwa na uongozi wa mkoa.
Maalim Seif aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa pendekezo la kutaka kurejeshwa kwa ngazi ya mkoa, lilizingatia haja ya kuunganisha na kuratibu shughuli za chama katika wilaya za mkoa husika.
Lakini wajumbe hao walijibu kuwa chama chao hakina uwezo wa kumudu gharama za uendeshaji kutokana na hali halisi iliyopo sasa. 
Mapendekezo mengine likiwemo la kurejeshwa kwa ngazi ya jimbo na kuwapo kwa Kamati ya Nidhamu na Maadili, yaliridhiwa. 
Jana, wajumbe hao walikuwa katika kipengele cha upigaji kura kuchagua viongozi wa ngazi za kitaifa, ambapo kwa matokeo ya awali kwenye nafasi ya mwenyekiti, Profesa Ibrahimu Lipumba alikuwa anaongoza. 


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru