Tuesday, 14 April 2015

Ajali zaua watu 103


NA WILLIAM SHECHAMBO
WATU 103 wamefariki na 138 kujeruhiwa kwenye ajali tisa za barabarani zilizotokea hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini.
Sababu kuu iliyoelezwa kusababisha ajali hizo ni uzembe wa madereva na abiria.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna Mohammed Mpinga, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kutoa tahadhari kwa abiria kutimiza wajibu wao ikiwa pamoja na kutowatetea madereva wazembe.
Alisema kikosi hicho kimeshitushwa na ajali zilizotokea mfululizo kuanzia Machi 11, mwaka huu, baada ya basi la kampuni ya Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, kuangukiwa na kontena na kusababisha vifo vya watu 50.
Kamanda Mpinga alisema hiyo ni idadi kubwa ya watu na upotevu wa nguvukazi ya taifa, ambayo pia iliongezeka kwenye ajali zingine nane zilizotokea maeneo tofauti na kufanya waliopoteza maisha kufikia 103.
Kutokana na ajali hizo, alisema wamewafutia leseni madereva wote waliosababisha ajali hizo zilizogharimu maisha ya Watanzania na kwamba wanaendelea na mikakati ya kutoa adhabu kali zaidi kwa wahusika wakiwemo wamiliki wa mabasi.
 Aliwataka wadau wa usalama barabarani kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kila basi linafika salama linakokwenda kwa kumwongoza dereva kuhusu mwendokasi.
Mpinga alisema mwendokasi kwa kiasi kikubwa umechangia ajali nyingi, ambapo madereva wamekosa hekima ya kutumia udereva wa kujihami kwa kutumia mabavu na ukorofi barabarani hasa kwa magari madogo, jambo linalosababisha ajali zinazoweza kuepukika.
Pia aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri, yakiwemo mabasi, kuwaongoza madereva wao kuzingatia sheria na taratibu za barabarani ikiwemo michoro ya alama ambazo zilichorwa kitaalamu kudhibiti matatizo barabarani, zikiwemo ajali.
Mpinga alisema hayo kutokana na uwepo wa madereva ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakipingana na sheria na kufanya wanavyotaka wawapo barabarani hasa kutokana na sababu kadhaa, hususan ulevi.
Alisema kikosi chake kitaendelea kusimamia sheria za usalama barabarani bila kuchoka ili kupunguza idadi ya ajali hapa nchini na hatimaye kuondoa kabisa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru