Tuesday 14 April 2015

Taasisi za dini kufutwa



  •  Ni zilizoshindwa kuwasilisha mapato na matumizi 
  •  Zingine zajiingiza kwenye siasa kinyume cha sheria 

NA MWANDISHI WETU 
TAASISI za dini ziko hatarini kufutwa katika orodha ya usajili kutokana na kuvunja sheria kwa kushindwa kutoa taarifa za mapato na matumizi ya hesabu za fedha kwa mwaka, imeelezwa.  
Kazi ya kuzifuta taasisi hizo,  inatarajia kufanyika Jumatatu ijayo, baada ya kukamilisha uchambuzi wa taasisi hizo na kwamba itaanzia jijini Dar es Salaam na baaadaye mikoani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu mustakabali wa nchi.

Alisema taasisi hizo ni zile ambazo hazifuati matakwa ya kisheria ikiwemo kuwasilisha taarifa za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada.
Chikawe alisema baadhi ya taasisi hizo ambazo zinakiuka sheria pia katika siku za hivi karibuni viongozi wa taasisi hizo, wamekuwa wakitoa matamko yanayoashiria kuingilia masuala ya kisiasa, kinyume cha sheria na katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
Waziri Chikawe alisema matukio hayo yamekuwa yakisababishwa na hamasa za kisiasa au baadhi ya watu waliokuwa wakitumia muda huo kutekeleza ajenda zao kwa kisingizio cha vuguvugu za kisiasa.
Alisema viongozi wa taasisi hizo wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi lakini ni kinyume cha sheria Sura ya 337, kutumia uongozi wao kushawishi waumini kutekeleza matakwa yao ya kisiasa.
Waziri alisema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakitoa matamshi ya kulenga na kushawishi wafuasi wao wafuate maelekezo yao kuhusiana na masuala ya Katiba Inayopendekezwa au kuhusu uchaguzi mkuu  wa Oktoba, mwaka huu.
“Matamshi haya yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo na hivyo serikali inatoa onyo kali kwa vikundi, zikiwemo taasisi hizo kuepuka kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu nchini,” alisema.
Pia katika mkutano huo, Chikawe alizungumzia suala la viongozi wa dini wanapochangisha pesa na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile kinachodaiwa kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbaliz za uongozi.
“Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni huku katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizi zinaeleza wazi kuwa kitendo hicho si kazi ya taasisi hizo,” alisema.
Alisema kuendelea kwa matukio hayo ya taasisi hizo kushiriki katika mambo ya kisiasa kunahashiria kuvurugika kwa amani na utulivu wa nchi.
Alisema matukio hayo yanahashiria uvunjifu wa amani na utulivu na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha taasisi hizo pamoja na viongozi wake wanadhibitiwa. 
Wiki iliyopita,Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,  Josephat Gwajima, alihojiwa kwa takribani saa sita katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalumu  ya Dar es salaam.
Gwajima alihojiwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa na matusi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, Februari, mwaka huu.
Kabla ya kufikishwa Kituo cha kati, alihojiwa katika  Kituo cha Polisi cha Oysterbay wiki mbili baada ya kuzirai akiwa kwenye kituo kikuu cha polisi na kupelekwa katika hospitali ya TMJ, Mikocheni kwa ajili ya matibabu. 
Mbali na kumhoji, polisi walimtaka kuwasilisha orodha ya mali zake, fedha alizo nazo katika benki tofauti, hati ya kumiliki helkopta, makanisa yake yote na ndugu zake walio hai na walio kufa.
Gwajima alitakiwa  kurudi tena kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kesho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru