Wednesday 22 April 2015

Watumishi mafisadi kitanzini



  •  Serikali yaibuka na mwongozo mpya
  •  Tume ya Maadili yapewa meno makali

NA WILLIAM SHECHAMBO
SERIKALI imeendelea na mikakati ya kuwadhibiti viongozi wa umma wanaokiuka maadili na kushiriki kwenye vitendo vya wizi na ufisadi, ambapo sasa imeunda mwongozo mpya utakaotumika kuwabana.
Mwongozo huo ambao unatajwa kuwa suluhisho na mwarobaini wa watumishi wezi na wanaokwenda kinyume, pia utaipa meno zaidi ya kiutendaji, Sekretari ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tofauti na ilivyo sasa.
Kwa sasa sheria na kanuni zinazoongoza maadili ya viongozi wa umma, lakini kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makusudi ama kusahau, baadhi ya viongozi wamekuwa wakizipuuza,  hivyo kusababisha matatizo ya kimaadili, hususan kuibuka kwa vitendo vya kifisadi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, mwongozo huo uko katika hatua za mwisho za maandalizi na utaanza kutumika kwenye mwaka wa fedha 2015/2016.
Mwongozo huo utaanza kutumia rasmi kabla ya kufanyika kwa matukio makubwa nchini, ikiwemo kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, ambao vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili vimekuwa vikishamiri.
Akizungumza kwenye warsha ya wadau ya kujadili rasimu ya mwongozo huo, Dar es Salaam, jana, Kapteni Mkuchika, alisema serikali ina nia madhubuti ya kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume na maadili.
Alisema kupitia mwongozo huo, jitihada za serikali kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2025, zinazosisitiza uongozi bora na utawala wa sheria, zinapewa nguvu kutokana na uwepo wa programu maalumu zinazohamasisha maadili  katika kila idara ndani ya sekta za umma na binafsi.
Mkuchika alisema mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaoota mizizi kote nchini, yanahitaji ushirikiano wa sekta zote, wananchi na asasi za kiraia,  ambapo adui mkubwa kati ya wengi ni rushwa na ufisadi, ambao kwa kiasi kikubwa unatekelezwa na viongozi wa umma.
Alisema maadili ya viongozi wa umma ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni pamoja na kukuza heshima ya taifa, hivyo serikali inafanya kila linalowezekana kutoa uwezo kwa Sekretarieti ya Maadili na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili matatizo hayo kutoweka nchini.,
Waziri huyo alisema nchi ilitikiswa na vitendo vinavyotokana na mmomonyoko wa maadili ya viongozi wa umma katika kipindi kifupi kilichopita, hali iliyoliletea aibu taifa na kuilazimu sekretarieti ya maadili kuwahoji watuhumiwa.
Waziri Mkuchika alisema ni lazima somo la maadili likaingizwa kwenye mitaala ya elimu kuanzia  shule za msingi mpaka elimu ya juu, ili kukomesha tatizo la ukosefu wa maadili kwa jamii, kwasababu utaratibu uliokuwa unatumika awali wa kupeleka vijana wote JKT kuwafundisha maadili kwa nyakati hizi hauwezekani.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema taasisi yake haitaendekeza vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kiongozi yeyote wa umma awapo kazini au atakapostaafu.
Alisema tangu kupatikana Uhuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kujenga na kukuza uadilifu kwa viongozi wa umma na sekta ya umma kwa kutumia sera, sheria, kanuni na miongozo, ukiwemo unaotarajiwa kutumika hivi karibuni.
Jaji Salome alisema kutumika kwa mwongozo huo ni mwendelezo wa juhudi hizo za serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo wakati huu wa kuelekea uchaguzi, viongozi husahau maadili na kufanya mambo kwa akili zao.
Alisema watapambana na kila kiongozi anayepotoka kimaadili kwa kutumia miongozo, kanuni na sheria, ili Tanzania iwe mahali salama kuishi kwa kuzingatia haki na usawa.
Aidha, alisema ili kuipa ‘meno’ sekretarieti ya maadili, serikali itaona namna ya kufanya  kuiruhusu imshitaki mtuhumiwa moja kwa moja mahakamani, wakiwemo wa ufisadi, badala ya kusubiri ruhusa kutoka kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP).
Sambamba na hilo, Mkuchika alisema Sekretari hiyo ambayo awali ilikuwa ni kitengo kidogo cha maadili ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), itapewa hadhi ya kuwa Tume, ili  ijitegemee  kama ilivyo kwa TAKUKURU.
“Taasisi hii ni muhimu sana, awali ilikuwa kitengo tu ndani ya jeshi; tukaona umuhimu wake tukakimegua ,ikawa na hadhi hii, sasa tumeona umuhimu wake zaidi kwa maendeleo ya maadili ya viongozi nchini, hivyo inabidi iwe tume, kama ilivyo TAKUKURU,” alisema Mkuchika. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru